Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakulima wabangladesh wateswa na mafuriko

Wakulima wabangladesh wateswa na mafuriko

Pakua

Nchini Bangladesh mabadiliko ya tabianchi yamekuwa ni mwiba kwa maisha ya kila siku ya watu wa taifa hilo la Asia. Kwa mujibu wa mfuko wa kimataifa wa maendeleo ya kilimo IFAD zaidi ya nusu ya watu milioni 90 wa nchi hiyo wanaishi katika maeneo yaliyoathirika vibaya na mabadiliko ya tabianchi huku wakikabiliwa na hatari kubwa ya mafuriko na wakulima ndio wanaobeba gharama kubwa ya zahma hiyo.

Taarifa ya Flora Nducha 

Katika eneo la Bhinnakury wilayani Sunamganji, picha za video zilizopigwa kutoka angani zinadhihirisha hali halisi ya janga la mabadiliko ya tabianchi , mafuriko kila kona huku nyumba zikionekana kuelea katika maji yaliyotokana namvua kubwa za monsoon zinazonyesha.

Mvua hizo zimesababisha vijiji kukatwa kabisa na mawasiliano kwani barabara zimefurika na hivyo kuwa mtihani kwa wakazi kupata huduma za msingi kama chakula kutoka sokoni, lakini pia kulima na kuhifadhi mavuno yao.

Nazrul Islam ni mkulima katika wilaya hii “Wakati wa mafuriko makubwa  kama haya mazao yetu yote yanafurika na kusambaratishwa, na hatuna nafasi za kutosha za kuhifadhi kwa usalama mazao tuliyovuna.” 
IFAD inasema mamilioni ya wakulima wadogo wadogo kama hawa kote duniani wanakabiliwa na changamoto kama hii kutokana na mabadiliko ya tabianchi yaliyochochea si ongezeko la majanga ya asili tu, bali pia kuongeza njaa na umasikini. 
Na ndio maana katika wiki ya pili ya mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi COP26 unaoendelea mjini Glasgow IFAD imetoa wito kwa serikali kuweka mahitaji ya wakulima wadogowadogo katika kitovu cha majadiliano ya ufadhili wa hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi ili kuwajengea mnepo.

Jyotsina Puri ni makamu wa Rais msaidizi wa IFAD anasema “Wakulima masikini pia ndio wanaohusika na na chakula chetu. Hivyo labda kwa maana ya ubinafsi tuwekeze kwao ili tuwe na chakula mezani. Theluthi moja ya chakula tunachopata na tunachokula huzalishwa na wao. Kwa ujumla ni muhimu zaidi kuwekeza kwa wakulima maskini wa vijijini kwa sababu kwao ni suala la kumudu kuishi. Na tusipowekeza kwao basi  hatutaweza kupata mnepo tunaotarajia kutoka kwa dunia hii." 

IFAD inasema hivi sasa ni asilimia 1.7 pekee ya ufadhili wa mabadiliko ya tabianchi, kionjo tu cha fedha zinazohitajika ndicho kinachokwenda kwa wakulima wadogowadogo na ukweli ni kwamba kiwango hicho hakitoshi.

Audio Credit
Assumpta Massoi / Anold Kayanda
Audio Duration
2'36"
Photo Credit
IMF/K. M. Asad