Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mauritania wapambana na mabadiliko ya tabianchi

Mauritania wapambana na mabadiliko ya tabianchi

Pakua

siku chache kabla ya kuanza kwa mkutano huo wa 26 wa nchi wanachama wa mabadiliko ya tabianchi, ambao hivi sasa unaendelea Glascow, Scotland, Mshauri Maalumu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudunia wakimbizi, UNHCR kuhusu Hatua dhidi ya Mabadiliko ya Tabianchi, Andrew Harper ametembelea Mauritania kujionea jinsi wakimbizi wanavyopambana na janga la tabianchi.

(Taarifa ya John Kibego)
“Hatujawahi kuona mwaka kama 2021. Huu ni mwaka wenye mioto mingi ya nyika.” Anasema Ahmedou El-Bokhary, Rais wa Kikosi cha zima moto kinachoundwa na wakimbizi.  

Andrew Harper, Mshauri Maalumu wa masuala ya hatua dhidi ya tabiachi kwa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, amejionea hali hiyo inayosemwa na anasema, “hii sio vita ambayo kunaweza kuwa na makubaliano ya amani nayo,” na anaongeza akisema, “Mauritania siyo tu ni mwenyeji wa maelfu ya wakimbizi, lakini moja ya nchi ambazo zimathiriwa zaidi na mabadiliko ya tabianchi.”

Yahya Koronio Kona yeye ni mkimbizi kutoka Mali anasema, “mito inapungua kina cha maji. Idadi ya samaki inakuwa ndogo, inasababisha matatizo.”

Bwana Harper anaendelea kueleza hali ilivyo mbayá akisema, "kuzunguka mito hii, kuna mifugo na hii mifugo inagombea vyanzo hivi vya maji. Na kwa hivyo moja ya changamoto kubwa sasa ni tuna ushindani kwenye rasilimali hizo zinazopungua, na maji pengine ni dalili zaidi ya changamoto za mabadiliko ya tabianchi. Na kwa hivyo tunatakiwa kufikiria kinachofuata.”

Wakimbizi wanasema wakati jua kali linapowaka, nyasi zinakauka na kushika moto. Na hapo kikosi chao cha kuzima moto kinaingilia kwani hawana namna nyingine.  

“Pamoja na changamoto zote,” anasema Bwana Harper, “pamoja na kile watu wanachofanya katika nchi za Magharibi kuiharibu dunia, watu wanaoteseka zaidi wanajaribu kufanya uamuzi sahihi ili kuyalinda mazingira na kutoa karibu muongozo ambao ni, ‘Kama tunaweza kufanya, kwa nini wengine duniani wasiweze?’”   

Audio Credit
Assumpta Massoi/ John Kibego
Audio Duration
2'5"