Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mnyama aliyetoweka mamilioni ya miaka atumika kuwakumbusha wanadamu kutochagua kutoweka

Mnyama aliyetoweka mamilioni ya miaka atumika kuwakumbusha wanadamu kutochagua kutoweka

Pakua

Mnyama aliyetoweka mamilioni ya miaka atumika kuwakumbusha wanadamu kutochagua kutoweka (OVERNIGHT)
Dunia ikiwa inaelekea katika mkutano wa tabianchi huko Glasgow, Scotland, Umoja wa Mataifa umemtumia "shuhuda" asiye wa kawaida kueleza hatari zinazoukabili ulimwengu ikiwa mienendo ya binadamu wa sasa ya kuharibu mazingira haitabadilika.

Taarifa ya Flora Nducha inafafanua kwa kina.

Filamu ya kwanza kabisa kutengenezwa ndani ya ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani kwa taswira iliyotengenezwa kwa teknolojia ya kompyuta, inaanza kwa kumwonesha mnyama aliyetoweka duniani takribani miaka milioni 70 iliyopita akiingia katika ukumbi huo kwa kishindo kikuu cha miguu yake iliyobeba mwili wake mzito. Hofu iliyowakumba wanadiplomasia walioko ukumbini inawafanya washindwe kunyanyuka kwenye vitia vyao...

Ni Dinosaria, mnyama mkubwa wa zamani anayeaminika kutoweka kutokana na majanga ya asili duniani anasimama kwenye mimbali ambayo hutumiwa na viongozi wa dunia kuhutubia ulimwengu,

Taswira hiyo ya bandia ya mnyama ni kitovu cha  kampeni ya shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa maendeleo, UNDP inayofahamika kama , “Usichague kutoweka” na ndio maana Dinosaria huyo kwa kutumia nadharia inayosemwa kuwa ndio ilimfanya kutoweka duniani, yaani uwepo wa vimondo vikubwa vilivyokuwa vikianguka duniani miaka hiyo, anawauliza wanadamu wa sasa wana kisingizio gani cha kuwafanya wao na viumbe wengine watoweke?
 
Anasema mamilioni yanatumika kuzipa ruzuku shughuli za uzalishaji wa mafuta ya kisukuku ambayo yanachafua hewa na kusababisha joto duniani wakati ulimwenguni kote watu wanaishi katika umaskini.
Dinosaria huyo anamalizia kwa kuwaambia wanadiplomasia waliotaharuki ukumbini kwamba, “ni wakati wa wanadamu kuacha visingizio vya kuanza kufanya mabadiliko. Kushughulikia janga la madabiliko ya tabianchi.”  

Audio Credit
Assumpta Massoi /Flora Nducha
Audio Duration
2'7"
Photo Credit
UNDP