Wapanda mlima kilimanjaro kuchangisha fedha za kupamba na COVID-19

Wapanda mlima kilimanjaro kuchangisha fedha za kupamba na COVID-19

Pakua

Wapanda mlima 34 leo wameanza safari ya kupanda mlima mrefu zaidi barani Afrika , mlima Kilimanjaro nchini Tanzania kama sehemu ya juhudi za kimataifa za kuchagiza upatikanaji wa chanjo ya COVID-19 kwa wote. Kundi hilo linalojumuisha watu kutoka katika nyanja za biashara, serikali, wanamichezo mashuhuri na wawakilishi wa vijana linatarajiwa kuwasili kwenye kilele cha mlima huo tarehe 24 Oktoba siku ya Umoja wa Mataifa. 
(TAARIFA YA FLORA NDUCHA) 

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa maendeleo UNDP, wapanda mlima hao kupitia mradi wa Kilimanjaro Initiatibve ,KI wanawakilisha tamaduni, uchumi, mazingira na mabara tofauti wakiwemo vijana 10 waliofadhiliwa kutoka miradi tofauti ya kijamii nchini Tanzania na shule za Tanzania na Kenya na pia wanawake wanariadha nyota wa mbio za milimani, viongozi wa kisiasa, maafisa wa Umoja wa Mataifa, madaktari, wanasayansi na wawakilishi wa vijana. 

Lengo lao kubwa kupanda mlima Kilimanjaro ni kuelimisha kuhusu haja ya haraka ya kuwa na usawa wa usambazaji wa chanjo dhidi ya COVID-19. 

Fedha zitakazopatikana wakati wa kupanda mlima zitakwenda kwenye  mfuko wa Muungano wa Afrika AU wa kupambana na COVID-19 na kampeni ya Go Give One inayosimamiwa na shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO.  

Na huko fedha zitatumika kutoa chanjo za COVID-19, huku kipaumbele kikitolewa kwa wanaozihitaji zaidi katika nchi ambazo haziwezi kumudu chanjo hiyo. 

Tim Challen, mwanzilishi wa NGO ya Kilimanjaro Innitiative (KI) iliyoandaa upandaji mlima huo au The Big Climb akimkunuu mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema "Kuelimisha kuhusu changamoto ya kutokuwepo haki ya upatikanaji wa chanjo ni muhimu ili kuleta suluhusho lenye usawa. Lazima tushirikiane kama familia ya kimataifa kupambana na COVID-19. The Big Climb inawakilisha mchango wetu katika juhudi hizi za pamoja. " 

Naye mmoja wa washiriki Dkt. Joseph Msaki wa hospitali ya Kilutheri ya Marangu nchini Tanzania amesema amehamasishwa sana na kiwango cha umakini na msaada wa kimataifa wa kutaka kumaliza janga la COVID-19 Afrika Mashariki . 

Amesema "Wakati tunaleta angalizo la kimataifa juu ya hitaji la chanjo za COVID-19  duniani, mradi huo pia umeleta vifaa muhimu kama barakoa, vifaa vya upimajia na paneli za sola kwa hospitali ya eneo letu," 

Madaktari wengine 3 kutoka India, Marekani na kundi la utafiti la ISGlobal wanashiriki katika kampeni hiyo sanjari na mwanariadha Mira Rai kutoka Nepal ambaye ni balozi mwema wa Umoja wa Mataifa wa ushirikiano wa milima na Akinyi Obama-Manners akiwakilisha vijana kutoka wakfu wa Auma Obama Sauti Kuu nchini Kenya. 

Wadau wengine wakubwa katika kampeni hii ni FAO mountain partnership, mfuko wa Benki ya Umoja wa Mataifa UNFCU, kituo cha Afrika cha kuzuia na kudhibiti magonjwa CDC, Muungano wa chanjo duniani GAVI, AU, mradi wa Women’s Brain na Sport and Sustainability International. 

Audio Credit
Assumpta Massoi / Flora Nducha
Audio Duration
3'8"
Photo Credit
UNICEF/Daniel Msirikale