Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yaridhia chanjo ya Malaria kwa watoto

WHO yaridhia chanjo ya Malaria kwa watoto

Pakua

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus akitangaza pendekezo la WHO la "matumizi mapana ya chanjo ya kwanza ya malaria ulimwenguni," amesema kuwa chanjo iliyosubiriwa kwa muda mrefu "ni mafanikio ya sayansi, afya ya mtoto na malaria." Taarifa ya Jason Nyakundi inaeleza zaidi. 

Kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Geneva Uswisi  Dkt Tedros akitangaza pendekezo la WHO la matumizi ya chanjo ya kwanza ya Malaria kutokana na matokeo ya programu inayoendelea ya majaribio nchini Ghana, Kenya na Malawi ambayo imewafikia zaidi ya watoto 800,000 tangu 2019, anasema, "Malaria imekuwa nasi kwa miaka elfu, na ndoto ya chanjo ya malaria imekuwa ndoto ya muda mrefu lakini isiyoweza kufikiwa. Leo, chanjo ya malaria ikifahamika kama RTS, S, zaidi ya miaka 30 ikifanyiwa utafiti  inabadilisha historia ya afya ya umma. Bado tuna barabara ndefu sana ya kusafiri. Lakini huu ni mserereko mrefu kuelekea chini kwenye barabara hiyo. Chanjo hii ni zawadi kwa ulimwengu, lakini thamani yake itaonekana zaidi barani Afrika, kwa sababu hapo ndipo mzigo wa malaria ni mkubwa zaidi." 

Mkuu huyo wa WHO akisisitiza umuhimu wah atua hii iliyofikiwa anasema, "leo ni siku ya kihistoria kwa sababu hii sio kwamba ni chanjo ya malaria tu, lakini pia ni chanjo ya kwanza ya ugonjwa wowote wa vimelea. Kwa hivyo, itafungua fursa kwa magonjwa mengine pia katika udhibiti wa magonjwa mengine pia. " 

WHO inapendekeza kwamba katika udhibiti kamili wa malaria, chanjo hii ya RTS, S / AS01 itumike kwa kuzuia malaria kwa watoto wanaoishi katika maeneo yenye maambukizi ya wastani hadi juu kwa vigezo vya WHO. Chanjo ya malaria ya RTS, S / AS01 inapaswa kutolewa kwa mpangilio wa dozi 4 kwa watoto w umri wa kuanzia miezi mitano.  

Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika Dkt Matshidiso Moeti anasema chanjo ya RTS, S ni "mabadiliko ya mchezo na inawasili wakati muafaka." Anasema maendeleo katika kupunguza mzigo wa malaria barani Afrika yamekwama katika miaka ya hivi karibuni, na zana na mbinu za ubunifu zinahitajika haraka ili kurudisha juhudi za kudhibiti malaria ulimwenguni. Pamoja na chanjo ya RTS, S na mabadiliko mengine yanayotarajiwa, tunatarajia kuona matokeo makubwa kwa mzigo wa malaria barani Afrika hivi karibuni." 

Malaria bado ni chanzo  kikuu cha magonjwa na vifo vya watoto katika eneo la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. Zaidi ya watoto 260 000 wa Kiafrika walio chini ya umri wa miaka mitano wanakufa kutokana na malaria kila mwaka. 

Audio Credit
Assumpta Massoi/Jason Nyakundi
Audio Duration
2'52"
Photo Credit
© UNICEF/Andrew Esiebo