Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakulima nchini Ethiopia wanufaika na mradi wa IFAD

Wakulima nchini Ethiopia wanufaika na mradi wa IFAD

Pakua

Mkutano wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa umefanyika hii leo jiijni New York, Marekani kando mwa mjadala mkuu wa mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA76 ambapo vioingozi wa nchi 193 wa Umoja huo wamejadili mifumo endelevu ya chakula ya kuwezesha wakulima kulima mazao bila vikwazo na vile vile kuzalisha vyakula vyenye lishe sambamba na kuongeza kipato.

Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa maendeleo ya kilimo, IFAD tayari umeshaanza kutekeleza mifumo ya aina hiyo ikiwemo huko nchini Ethiopia ambako ujenzi wa mfereji wa umwagiliaji umeleta nuru kwa wakulima kama anavyosimulia Anold Kayanda

(Taarifa ya Anold Kayanda/Assumpta Massoi)
Temesgen Chanie  [CHEN] mkulima wa ngano na viazi mbatata akiwa kwenye konde la ngano. Yeye alikuwa akijipatia fedha kwa kulima chakula lakini mabadiliko ya tabianchi yalimaanisha kuwa hakuweza kulisha  familia yake kwa mwaka mzima.

Uhaba wa mvua na vipindi virefu vya ukame ndio sababu ya mavuno hafifu kutoka shambani mwake na hivyo kulazimika kulima mazao yanayohitaji kiwango kidogo cha maji.

Hata hivyo mwaka jana wa 2020, kila kitu kilibadilika akisema “Kama familia sasa tunakula aina tofauti za vyakula,  ukilinganisha na awali ambapo tulikula aina moja ya chakula iwe asubuhi, mchana au usiku.” 

Mabadiliko hayo yanafuatia ujenzi wa mfereji mpya wa umwagiliaji katika kijiji chao ukinufaisha zaidi ya kaya 200 za wakulima na hivyo kuwawezesha kulima mazao mbalimbali kwa kipindi cha mwaka mzima. “Mfereji huu  umetuwezesha kulima kwa kiasi kikubwa matunda na mboga za majani. Tunaweza hata kununua vyakula vingine madukani.”

Ukifadhiliwa na mfuko wa Umoja wa Mataifa wa maendeleo ya kilimo, IFAD kwa kushirikiana na serikali ya Ethiopia , mfumo huo wa umwagiliaji ni sehemu ya miradi ya kuwezesha wakulima wadogo kukabiliana na athari hasi za mabadiliko ya tabianchi.

Ili kuwezesha wakulima kuendelea na shughuli zao hata wakati wa janga la Corona au COVID-19, fedha nyingine za mradi zimeelekezwa katika kuwapatia mbegu za mazao zinazohimili ukame sambamba na mbinu bora za kilimo.

Vyote hivyo vimeongeza tija kwa wakulima na lishe bora kwa familia zao. Angach Mekonnen ni mkulima wa mahindi na viazi na anasema, “Sasa napatia familia yangu mboga za majani, viazi, kunde na maharage kwa kiasi kikubwa kuliko hapo awali. Zamani sikuweza hata kuwapatia supu ya kutosha ya Shiro.”

IFAD inalenga kutoa mafunzo kwa wakulima wengi zaidi pamoja na mbinu za kilimo hifadhi ili hatimaye wakulima wanufaike siyo tu kwa lishe bora bali pia kipato.

Audio Credit
Assumpta Massoi/Anold Kayanda
Audio Duration
1'39"
Photo Credit
Unsplash/Jeremy Zero