Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mjadala Mkuu wa UNGA76 wafungua pazia New York

Mjadala Mkuu wa UNGA76 wafungua pazia New York

Pakua

Mjadala Mkuu wa ngazi ya juu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UNGA76 leo umeng’oa nanga rasmi katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa hapa jijini New York Marekani ukifanyika moja kwa moja na pia kupitia mtandaoni ukiwaleta pamoja nchi 193 wanachama wa Umoja huo.

Flora Nducha na taarifa zaidi 
Abdullah Shahid Rais wa Baraza Kuu akifungua mjadala huo ambao umebeba mada ya “Kujenga mnepo kupitia tumaini la kujikwamua kutoka kwa janga la COVID-19,  kushughulikia mahitaji ya sayari dunia, kuheshimu haki za watu, na kuufufua Umoja wa Mataifa. " 

Hii ni mara ya pili mjadala huu unafanyika wakati janga la COVID-19 likiendelea tofauti na mwaka jana ambapo kwa asilimia kubwa ulifanyika kwa njia ya mtandao mwaka wakuu wa nchi za serikali wachache wanashiriki kupitia mtandao na wengine takriban 100 wako moja kwa moja kwenye ukumbi wa Baraza Kuu akiwemo Katibu Mkuu Antonio Guterres ambaye amesema.  

“Niko hapa kupiga kengele ulimwengu lazima uamke. Tuko ukingoni mwa dimbwi na tunaenda katika mwelekeo mbaya. Ulimwengu wetu haujawahi kupata tisho zaidi ya hili au kugawanywa zaidiya sasa. Tunakabiliwa na mtafaruku mkubwa katika maisha yetu. Janga la COVID-19 limezidisha pengo la usawa, mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi unaipiga dunia, machafuko kutoka Afghanistan hadi Ethiopia hadi Yemen na kwingineko yamezuia upatikanaji wa amani.” 

Ametaja changamoto zingine kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa hali ya kutoanimiana duniani, kuendelea kubinywa kwa haki za binadamu, kushanmbuliwa kwa sayansi na migongano ya kiuchumi. Kwa upande wa janga la COVID-19 amesema hakuna mshikamano kwa vitendo, wakati huu ambao unahitajika kuliko wakati mwingine wowote, kwani ubinafsi umetawala na utu umetoweka 

"Taswira tuliyoiona katika baadhi ya nchi kuhusu chanjo ya COVID-19 , ziko majalalani, muda wake umekwisha na hazijatumika. Na kwa upande mwingine tunashuhudia chanjo zikizalishwa kwa kasi isiyo ya kawaida, ambao ni ushindi wa kisayansi na ujuzi wa kibinadamu.. Lakini kwa upande mwingine tunaona ushindi huu ukisambaratishwa na janga la kutokuwa na utashi wa kisiasa, ubinafsi na kutoaminiana. Kuna ziada katika baadhji ya nchi , wakati kwingineko hawana chochote, watu wengi katika nchi Tajiri wamechanjwa, lakini zaidi ya asilimia 90 ya Waafrika bado wanasubiri dozi ya kwanza. Haya ni mashtaka ya kimaadili ya hali ya ya dunia yetu. Ni uchafu, tumefaulu mtihani wa sayansi, Lakini tunapata F katika maadili.” 

Amesisitiza kwamba huu ni wakati wa kutambua mbivu na mbichi, wakati wa kutekeleza kwa vitendo, wakati wa kurejesha uaminifu , wakati wa kuchagiza matumaini, kwani yeye anayo matumaini .  Ametaja mambo sita ya kuzingania ambayo mosi ni kuhakikisha kuna amani, pili lazima kupata kushikimana dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, tatu lazima kuziba pengo la baina walionacho na wasio nacho, nne lazima kumaziba pengo la usawa wa kijinsia, tano kurejesha uaminifu na kuchagiza matumaini na sita lazima kuziba pengo baina ya vizazi.

Naye  Rais wa Baraza Kuu Abdulla Shahid katika hotuba yake ametaja mambo matano muhimu kuweza kukabiliana na changamoto zote zinazoikabili dunia kwa hivi sasa akisema 

Kama ulivyo utaratibu wa kila mwaka katika mjadala wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa Rais wa Brazil Jair Bolsonaro amekuwa mjumbe wa kwanza kuwasilisha taarifa yake akifuatia na Rais Joe Biden wa Marekani , lakini nchi zote wanachama zinatarajiwa kuzungumza katika mjadala huo utakaojikita pia katika masuala ya kumbukumbu ya miaka 20 ya azimio la Durban, mifumo ya chakula, nishati, mabadiliko ya tabianchi na kumuenzi aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Dag Hammarskjöld.

Audio Credit
Assumpta Massoi/ Flora Nducha
Audio Duration
4'52"
Photo Credit
UN Photo/Evan Schneider