Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukosefu wa maji safi wasababisha UNMISS kuanzisha doria ya kufuata maji msituni

Ukosefu wa maji safi wasababisha UNMISS kuanzisha doria ya kufuata maji msituni

Pakua

Kwa kutambua ukosefu wa usalama na uhaba wa maji unaowakabili wakimbizi wa ndani walioko Tambura nchini Sudan Kusini, walinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini humo wameanzisha doria maalum ya kuwasindikiza wakimbizi hao kuteka maji  maji ili kuwahakikishia usalama katika kusaka rasilimali hiyo adhimu. 

(Taarifa ya Leah Mushi) 
Jimboni Equatoria Magharibi nchini Suda Kusini, video ya mpango wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Sudan Kusini UNMISS inaonesha mwanajeshi aliyevalia kofia ngumu ya buluu, rangi ya Umoja wa Mataifa akiwa ameshika bunduki akitembea, nyuma yake akifuatiwa na kundi kubwa la watu waliobeba madumu ya maji, na nyuma ya kundi hilo linafuata gari na mwanajeshi mwingine mwenye bunduki. 

Hii ni doria maalum, si kama zile za kuwasaka wavunjifu wa amani, bali ya kuhakikisha usalama wa raia wanaoenda kuteka maji, na mkimbizi wa ndani Margret Albert anashukuru wanavyosindikizwa.  
 
“Tunashukuru kwa kile walinda amani wanafanya kutusindikiza kusaka maji. Tunaogopa kwenda msituni peke yetu. Lakini wanapotusindikiza, tunahisi tumelindwa. Ni jambo zuri ambalo wanafanya. Wanapotusindikiza wakati wa mchana, tunaweza kuteka maji na kukabiliana na uhaba wa rasilimali hii ya thamani”. 
 
Hata hivyo idadi kubwa ya wakimbizi hawa wana wasiwasi mkubwa juu ya ukosefu wa maji safi na salama ya kunywa kama anavyoeleza Leticia Mario Sasa. “Maji tunayokunywa ni machafu. Tunahofia  kwamba kesho au siku inayofuata sisi sote tutaugua. Watoto wetu na sisi sote tutakuwa wagonjwa na kuanza kufa. Tunaishi katika mazingira yenye msongamano mkubwa, hatupati hewa safi na hatuwezi kuishi mbali kwa sababu tunaogopa. “ 
 
Mpaka sasa zaidi ya wakimbizi wa ndani 40,000 wengi wao wakiwa ni wanawake na Watoto wako chini ya uangalizi wa walinda amani wa UNMISS katika maeneo matatu ndani ya eneo la Tambura. 
 
Afisa wa masuala ya raia Farai Nyamayaro anasema dhamira yao ni kuwahakikishia usalama wananchi na kuzuia vurugu zaidi. “Lengo la UNMISS [UNMIS]  siku zote limekuwa ni kuingilia kati kuokoa maisha. Kile ambacho tumejikita nacho kimsingi ni kujaribu kutuliza vurugu, lakini wakati huo huo kuwapa ulinzi wakimbizi wa ndani. Tunayo  maeneo matatu ambayo tunatoa ulinzi, na ndani ya maeneo hayo kumekuwa na mahitaji ambayo tunajaribu kuyashughulikia. Tumefanya doria za kwenda kuteka maji ambapo tunaongozana na wakimbizi wa ndani kuteka maji kutoka vyanzo vya maji vilivyopo karibu. Zaidi ya hayo, tumekuwa pia tukijaribu kuzungumza na viongozi wa serikali wa ngazi za juu pamoja na maafisa wengine wa jeshi ili waweze kufika hapa na kusaidia kumaliza ghasia eneo hili.” 

Audio Credit
Assumpta Massoi/Leah Mushi
Audio Duration
2'53"
Photo Credit
UNMISS