Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yatoa muongozo wa vyeti vya chanjo ya COVID-19 kielektronik

WHO yatoa muongozo wa vyeti vya chanjo ya COVID-19 kielektronik

Pakua

Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO linasema ingawa haliungi mkono mahitaji ya uthibitisho wa chanjo ya COVID-19 ili mtu kuweza kusafiri lakini katika mazingira mengine kulingana na tathmini ya hatari ya nchi zinazohusika, taarifa kuhusu chanjo dhidi ya COVID-19 zinaweza kutumika kupunguza mahitaji ya karantini au upimaji wakati wa kuwasili katika nchi hizo. 

(Taarifa ya Anold Kayanda) 

Kutokana na msingi huo wa umhimu wa kutunza taarifa za chanjo, hivi karibuni WHO imetoa waraka wenye mwongozo kwa nchi duniani na wadau wengine kuhusu mahitaji ya kiufundi kwa ajili ya kutoa vyeti vya kidijitali vya chanjo dhidi ya Covid-19. 

Mwongozo huo ni sehemu ya mfululizo wa nyaraka kuhusu kuweka vyeti vya Covid-19 katika mfumo wa kidijitali. Na mwongozo huo, pamoja na mambo mengine, utayasaidia mataifa wanachama katika kuidhinisha zana za kidijitali za kuhifadhi taarifa ya chanjo ya COVID-19 kwa madhumuni ya huduma bora za afya, na uthibitisho wa chanjo ikiwa itahitajika kwa madhumuni mengine. 

Ingawa WHO inaeleza kuwa lengo kuu la mwongozo huu sio kuelekea katika nyaraka za kidijitali za hali ya COVID-19 lakini vyeti vya chanjo sio kitu kipya duniani kwani ni hati za afya ambazo zinarekodi tukio la chanjo, kijadi kama kadi ya karatasi na maelezo muhimu ikiwa ni pamoja na tarehe, namba ya chanjo na aina ya chanjo ambayo mtu amepatiwa.  

WHO inasema kuweka taarifa za Covid-19 katika mfumo wa kidijitali, kunapendekezwa kama utaratibu ambao taarifa za afya zinazohusiana na COVID-19 zinaweza kuhifadhiwa kidijitali kupitia cheti cha kielektroniki. 

Kihistoria, rekodi za chanjo katika karatasi zimekuwa na changamoto nyingi kama uwezekano wa kupoteza au kuharibika kwa kadi, au hata uwezekano wa ulaghai. Ufumbuzi uliopendekezwa wa kidijitali umeundwa kushughulikia changamoto hizi. 

Audio Credit
Grace Kaneiya /Anold Kayanda
Sauti
1'43"
Photo Credit
WHO-Europe