Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkimbizi asimulia alivyokatwa sikio na kutakiwa kulila

Mkimbizi asimulia alivyokatwa sikio na kutakiwa kulila

Pakua

Kijana Gatwech mkimbizi wa ndani akiwa katika kambi muda ya wakimbizi kwenye  ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani Sudan Kusini UNMISS anasimulia madhila wanayokutana nayo wakimbizi ambapo yeye kabla ya kukimbia usiku kucha ili kuokoa maisha yake alikatwa sikio na kutakiwa kuliokota alile. Ungana na Leah Mushi kwa simulizi zaidi.

(Taarifa ya Leah Mushi)
 Kwa wiki kadhaa kituo cha ulinzi wa raia kilicho chini ya UNMISS mjni Yambio kimekuwa kikipokea makundi ya watu kutoka Tambura, jimbo la Equatoria magharibi nchini Sudan Kusini wanaokimbia vijiji vyao baada ya kuvamiwa na watu wenye silaha ambao wamechoma makazi yao na kuua raia.

Akiwa ameketi hapa kituoni Yambio, huku akivibinya vidole vyake kijana Gatwech ambaye sio jina lake halisi, baba wa mtoto mmoja anasimulia madhila yaliyomfika huko Tambura.
“Walitokea ghafla na kunielekezea bunduki, wakaniamuru niketi. Walituvua viatu na kuanza kutoa mali na kutupeleka Nabiama. Walinikata sikio na kumuua ndugu yangu John. Niliogopa sana, wakati nilisikia kisu kikiwa sikioni kwangu. Walilikata, wakalitupa chini na kuniuliza ikiwa nitalila sasa hivi. Mshambuliaji mwingine alitudhihaki kwa kutuuliza ikiwa watuchinje mahali pamoja, chini ya mti mkubwa. Dakika hiyo niliposikia hivyo, nilijua watatuua, na ni bora kukimbia kuliko kupigwa risasi hadi kufa. Nilipoanza kukimbia, nilisikia watu watatu wakipiga kelele; mayowe yalikoma ghafla. Nilitembea usiku kucha mpaka kufika kuripoti polisi. Jambo bora tunaloweza kuwa nalo kwa sasa ni amani. Tumeishi kwa muda mrefu sana na mizozo na mashambulio."
 
Mkuu wa ofisi ya UNMISS mjini  Yambio, Christopher Murenga anasema wao wanafanya juhudi na kutoa wito kwa serikali ya Sudan Kusini. "Tunasisitiza kuwa ulinzi wa raia na utoaji wa msaada kwao ni jukumu la msingi la serikali. Sisi kama Umoja wa Mataifa tuko hapa kuunga mkono hilo, lakini kwa kweli wanahitaji kuchukua jukumu la kulinda raia wao,  kutuliza hali, kupunguza vurugu na kushirikisha pande zote zinazogombana katika mazungumzo kama njia ya kumaliza shida ambazo tunakabiliwa nazo kwa sasa katika kaunti ya Tambura, ili kuhakikisha amani na utulivu wa kudumu vinapatikana na hatimaye  raia hawa waweze kuendelea na maisha yao ya kila siku. ”

Pamoja na kuomba amani lakini kuna madhila mengi yanawakumba wakimbizi hawa kama anavyoeleza afisa wa haki za binadamu wa UNMISS Leticia Marino. "Ni wazi kwamba tunazungumza juu ya watu waliouawa na wengine wamepotea na ambao wanafamilia wao wanawatafuta sana. Tunazungumza juu ya upotezaji mkubwa wa mtaji, tunazungumza juu ya mazao ambayo yameharibiwa na ni hali hii inaweza kuleta mgogoro wa chakula ambao ni dhahiri unakaribia hapa katika Ikweta ya Magharibi. Tunazungumza juu ya shida kubwa ya kibinadamu na hasara kubwa kwa mchakato wa amani kwa Sudan Kusini. "

Wiki iliyopita mamia ya watu walijumuika kwenye ibada ya kijamii ya kuomba amani iliyoandaliwa na vikundi vya dini vya Equatoria magharibi ikiwa ni juhudi ya kutafuta amani na kumaliza machafuko katika eneo hili ambalo awali lilitegewa kwa kilimo.

Audio Credit
Assumpta Massoi/Leah Mushi
Sauti
3'20"
Photo Credit
UN Photo/Gregorio Cunha