Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa zaidi ya dola milioni 44 waleta mafanikio nchini Uganda

Mradi wa zaidi ya dola milioni 44 waleta mafanikio nchini Uganda

Pakua

Nchini Uganda mradi wa kurejesha maeneo oevu ambayo yalikuwa yanatoweka kutokana na shughuli za binadamu umeanza kuzaa matunda kwa kuwa sasa maeneo yamenusuriwa na wananchi wanapata kipato bila kuharibu mazingira. 

(Taarifa ya John Kibego)
Ukubwa wa eneo oevu nchini Uganda limepungua kwa kiasi kikubwa kutoka asilimia 15.9 mwaka 1994 hadi asilimia mwaka 2019 kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo shughuli za binadamu.

Maeneo oevu ni muhimu kwani pamoja na mambo mengine hufyonza hewa ya ukaa, huchuja maji,  huzalisha chakula na huzuia mafuriko.
Ni kwa kuzingatia hilo, serikali ya Uganda kwa ushirikiano na Umoja wa  Mataifa wanatekeleza mradi wa miaka minane kuanzia mwaka 2017 hadi 2025 ambapo wananchi wanapatiwa mbinu mbadala za kujipatia kipato ili kurejesha maeneo oevu.

Mradi una thamani ya dola milioni 44.2 na unatekelezwa katika wilaya 24 za kusini magharibi na mashariki mwa Uganda. 
Kati ya fedha hizo dola milioni 24.1 zinatoka mfuko wa tabianchi wa Umoja wa Mataifa, dola 18.4 ni za serikali ya Uganda ilhali dola milioni 2 zinatoka UNDP.

Wanufaika kama Mary Amoding walipatiwa mitamba ya ng’ombe na anasema,  “ng’ombe huyu atanisaidia kwa njia mbalimbali. Mosi nikiuza maziwa naweze kumjenga banda lake na fedha zinazobakia najilisha, najivisha na kujikimu mahitaji yangu mengine.“
Katika wilaya ya Mitooma, kikundi cha Nshenga Abatengane chenye wanachama 48 wakiwemo wanawake, wanaume, vijana na wazee. Katika kipindi cha miaka mitatu kila mwanakikundi alikuwa ameshapatiwa watoto wawili wa nguruwe.

Milton Mikiranabo ni mwenyekiti na shuhuda wa mafanikio ya mradi huu akisema, “wanachama niliwapatia nguruwe watatu watatu. Na nimeona mafanikio. Mosi, nimeuza na kulipia karo ya elimu kwa watoto wangu, na pili nimetumia samadi yao kurutubisha miti ya matunda.”

Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Mazingira Alfred Okodi Okot anasema mradi umenusuru maeneo oevu.“Tumeona maeneo oevu yamarejea, viumbe ambavyo vilihama iwe wanyama, ndege au nyoka, sasa vimerejea. Pia jamii zinazoishi kando mwa maeneo oevu wanapata kipato zaidi kuliko awali walipotumia maeneo oevu moja kwa moja. Hapo ndio tunasema bayonuai na binadamu viko pamoja kwa amani.”


 

Audio Credit
Assumpta Massoi / John Kibego
Audio Duration
2'28"
Photo Credit
©FAO/Luis Tato