Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanamichezo wakimbizi wanaoshiriki Olympiki watumiwa salamu za heri na familia zao

Wanamichezo wakimbizi wanaoshiriki Olympiki watumiwa salamu za heri na familia zao

Pakua

Wanamichezo wakimbizi wanaoshiriki katika michuano ya Olympiki Tokyo Japan wametumiwa salamu za heri na familia zao zilizoko katika kambi ya wakimbizi ya Kakuma nchini Kenya.  Hiyo ni kwa mujibu wa video ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR.

(Taarifa ya Leah Mushi)

Kambini kakuma nchini Kenya wakimbizi wa kutoka Sudan kusini wakitazama video kupitia simu za mkononi kujikumbusha wakati wanamichezo wakimbizi walipokuwa wakifanya mazoezi kabla ya kufuzu kwenda kwenye michuano ya olimpiki Tokyo nchini Japan.

Wanamichezo 29 wanapeperusha bendera ya wakimbizi katika michezo 12 ikiwemo riadha, miongoni mwao ni Rose Nathike na wazazi wake wanamtakia heri binti yao. “Mungu akujalie moyo safi, kimbia nao, kimbia kama kawaida, na ninakuombea upate nafasi ya kwanza ili utakaporudi, sote tushereehkee Ushindi wako”

Baba Mzazi wa Rose, John Lokonye naye hayuko nyuma akisema,“Ninaomba kwamba Mungu akusaidie kufanya vizuri, na urudi na kitu kizuri”

Mwanariadha mwingine ni Angelina Lohalith alikimbia vita nchini Sudan kusini akiwa na umri wa miaka 6 tangu kipindi hicho hajawahi kuwaona wazazi wake, lakini kambini anaishi na ndugu zake akiwemo mdogo wake aitwaye Regina Nakang Aloitho. Regina anamwambia dada yake usiwe na hofu maana hii ni mara yako ya pili kushiriki mashindano ya Olimpiki, “Ninafurahi sana, naomba tuu Mungu asaidie yeye, lakini yeye asikuwe na haraka acha tuu akimbie vile Mungu alikuwa anasaidia yeye “

Kakuma inahifadhi wakimbizi kutoka Sudan Kusini n ani eneo ambako vipaji vyao vya kukimbia viligundulika na tangu hapo wamekuwa wakipatiwa mafunzo kambini Kakuma na kituo cha michezo Ngong kilichoko karibu na mji mkuu wa Kenya, Nairobi, kabla ya kwenda katika mashindano ya Olimpiki nchini Japan.

Audio Credit
Assumpta Massoi/Leah Mushi
Audio Duration
1'58"
Photo Credit
UN News/Jing Zhang