Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bhutan imefanikiwaje kutoa chanjo kwa asilimia 90 kwa wananchi wake?

Bhutan imefanikiwaje kutoa chanjo kwa asilimia 90 kwa wananchi wake?

Pakua

Kiwango cha utoaji wa chanjo dhidi ya ugonjwa wa Corona au COVID-19 nchini Bhutan huko barani Asia kimefikia asilimia 90 ya wananchi wote wenye umri wa kupatia chanjo hiyo. Kampeni ya utoaji chanjo imefanywa na serikali ya Bhutan kwa ushirikiano na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF.  
 
(Taarifa ya Leah Mushi) 
 
Video ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF inaanza kwa taswira ya Bhutan, nchi iliyozungukwa na milima ya himalaya ikiwa na eneo lisilozidi kilometa elfu 40 na imepakana na India na China. 
 
Wahudumu wa afya wakiwa wamevalia mavazi mahususi ya kujikinga na Corona wakiwasili na chanjo kwa ajili ya kupatia wananchi ambao tayari wako kwenye msururu. 
 
Akizungumzia kampeni hii ya chanjo dhidi ya Corona, Mwakilishi wa UNICEF nchini Bhutan, Dkt. Will Parks amesema, “tunaipongeza serikali ya kifalme ya Bhutan, kwa kukamilisha awamu ya pili ya kampeni ya kutoa chanjo nchi nzima. Matokeo ya kazi nzuri ya serikali ni asilimia 90 ya watu wote walio katika umri wa kupatiwa chanjo nchi nzima wamechanjwa. Na bado zoezi la utoaji chanjo kwa watu wakiwa majumbani linaendelea mpaka julai 31, bilashaka kutakuwa na ongezeko la waliochanjwa wiki chache zijazo.”  
 
Uongozi mahiri wa mfalme wa nchi hiyo, Je Khenpo kwa kushirikiana na viongozi wenzake, vijana na wadau wa maendeleo, vinaelezwa kuwa ndio nguzo ya mafanikio hayo, ambapo watoa huduma 2401 walitawanywa milimani kuwapatia chanjo wananchi. 
 
UNICEF kama mdau, imesaidia katika kutoa majokofu ya kuhifadhi chanjo, kuwezesha usafirishaji wa chanjo kwa haraka ikiwemo kutumia helikopta huku watoa chanjo wakipatiwa mikoba yenye uwezo wa kuhifadhi baridi wakati wanafuata watu majumbani kwa ajili ya chanjo ya COVID-19. 

Bhutan imepata chanjo kupitia mfumo wa Umoja wa Mataifa wa mgao wa chanjo, COVAX ikiwa ni msaada kutoka Marekani, China, Denmark na India. 
Bhutan imekuwa mfano wa nchi yenye kuleta matumaini, kwa kufanikiwa kwa shughuli nzima ya utoaji chanjo, ikionesha ni namna gani nchi zinavyoweza kujilinda na hatari za janga la corona linalozidi kugharimu maisha ya watu na kuziacha familia katika mashaka makubwa.

 

Audio Credit
Grace Kaneiya /Leah Mushi
Sauti
2'9"
Photo Credit
© UNICEF Bhutan/Tshering