Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi zakumbushwa kuanzisha vituo vya taarifa na udhibiti wa sumu

Nchi zakumbushwa kuanzisha vituo vya taarifa na udhibiti wa sumu

Pakua

: Sumu ni tatizo la afya ya umma lakini bado nchi zinapuuza kuweka vituo vya kudhibiti
Duniani kote tatizo la binadamu kukumbwa na sumu halipatiwi kipaumbele au hata haliripotiwi kuwa ni tatizo la afya la umma. Llicha ya kwamba shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO linapendekeza kila nchi kuwa na vituo vya kufuatilia na kutibu bado ni chini ya nusu ya wanachama 194 wa shirika hilo wana vituo hivyo na miongoni mwao ni Thailand.

(Taarifa ya Grace Kaneiya)
Nchini Thailand kuna wagonjwa zaidi ya 15,000 kila mwaka wanaokuwa wamekumbwa na sumu. WHO inasema hatua ya haraka ya kudhibiti kuenea sumu mwilini na pia kutibu ni muhimu ili mgonjwa aweze kupona.
Katika mji mkuu wa Thailand, Bangkok, kituo cha Ramathibodi cha kutoa taarifa kwa njia ya simu kwa waathirika wa sumu kilifunguliwa mwaka 1996 kusaidia kinga, uchunguzi na usimamizi wa tatizo la sumu.

Kituo hiki kina watendaji walio kwenye kompyuta pamoja na simu. Charuwan Sriapha ni Mkuu wa taarifa za kisayansi katika kituo hicho.
"Simu inapoita, tunaanza kupokea taarifa, je mgonjwa alikumbwa na sumu ipi, dalili ni zipi na daktari amebaini nini.?”

Kituo kinafanya kazi saa 24, siku 7 kwa wiki na wafanyakazi wanajibu maswali kuhusu sumu za aina mbalimbali iwe nyoka au dawa za kuulia wadudu na kadhalika na kisha wanatoa taarifa iwapo sumu hiyo ni hatari au la na aina ya tiba inayotakiwa iwapo ni lazima.
"Tunatathmini iwapo mgonjwa anaweza kwenda eneo la kupata tiba, yaani hospitali au mgonjwa apelekewe dawa, yaani hospitali husika ipeleke dawa nyumbani kwa mgonjwa.”

Mgonjwa kupata dawa kwa wakati ni hatua inayookoa maisha. Mwaka 2020, kitu cha Ramathibodi kilihudumia zaidi ya wagonjwa wa kipekee 29,000, na zaidi ya nusu sumu zao zilihusiana na dawa na viuatilifu.

Miongoni mwa manusura ni Kittithee, mtoto huyu ambaye akiwa na umri wa miaka 7 aliifkishwa kituo cha Ramathibodi baada ya kupigwa risasi ya mguu. Alipooza na zaidi ya hapo damu yake ilikuwa na viwango vya juu vya madini ya risasi kwa sababu ya risasi aliyofyatuliwa.
Mtaaamu wa sumu kituoni Ramathibodi Dkt. Satariya Trakulsrichai anafafanua kuwa mtoto huyo alipatiwa tiba kwa miaka kadhaa na kupunguza athari ya sumu mwilini. "Leo hii inaweza kutembea na kufanya shughuli zake. Anaweza kwenda shuleni, anaweza kuota ndoto na anataka kuwa mhasibu akikua. Anaishi tena maisha ya utoto.”

Kituo cha Ramathibodi kinachofanya kazi kwa ushirikiano na WHO, ni mfano wa jinsi vituo vya kudhibiti sumu vinaweza kuwa na athari chanya katika siyo tu nchi moja bali ukanda kwa kuwa kituo hiki kinaratibu usambazaji wa tiba za sumu Kusini-Mashariki mwa Asia.
TAGS: Sumu, WHO, Ramathibodi, Thailand
 

Audio Credit
Assumpta Massoi / Grace Kaneiya
Audio Duration
2'35"
Photo Credit
UNEP