Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa Mfereji wa Maji waboresha maisha ya wakazi wa Kabul, Afghanistan

Mradi wa Mfereji wa Maji waboresha maisha ya wakazi wa Kabul, Afghanistan

Pakua

Kila siku wananchi watano katika kijiji cha Pazhaki jimboni Kabul nchini Afghanisan walikuwa wanajukumu la kufungulia maji katika mfereji uliokuwa unategemewa na wanakijiji hao kwa shughuli za kilimo. Lakini Ramazan Ibrahimkil, mwenyekiti wa Kijiji cha Pazhak anasema alikuwa anapokea kesi kila uchwao kwamba wananchi wanaokaa milimani wakilalamikiwa kufungulia maji kwa wingi na hivyo wale wa mabondeni kukosa maji ya kutosha kwenye kilimo chao na hivyo kupata mazao machache na kipato kidogo. 

Benki ya Dunia kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo ya Afghanistan imekarabati mfereji wa zamani na kuweka usimamizi mzuri na sasa wananchi wote wanafurahi na kipato kimeongezeka. Mamia ya wakulima wa Afghanistan katika jimbo la Kabul kwa sasa wanazalisha mazao mengi na kupata kipato kikubwa shukrani zikienda kwenye mradi wa umwagiliaji kwa kutumia mfereji waliokuwa wanautegemea kwa kilimo ambao sasa umefanyiwa marekebisho na Taasisi inayosimamia kujenga upya Afghanistan kifupi, ARTF, ambayo inapata fedha kutoka Benki ya Dunia na wahisani wengine. 


Ramazan anasema kesi zilizidi. “Tatizo kubwa kwenye jamii yetu ilikuwa ni usambazaji wa maji, malalamiko yalikuwa yalikuwa yanaletwa sababu wakulima walioko maeneo yenye muinuko kwa uhalisia wanapata maji mengi, wakati wale walioko sehemu za mabondeni walikuwa wakilalamika ardhi yao haipati maji ya kutosha. Nilikuwa nalazimika kuja huku kila siku kusuluhisha hizi kesi, kitu ambacho kilikuwa kinapoteza sana muda na nguvu ya kila mtu aliyekuwa akishiriki katika usuluhishi.”


Wakulima kutoka Kijiji cha Pazhak wanashirikiana kuruhusu kuhusu maji kupita kwenye mfereji huo ulioboreshwa wenye urefu wa kilometa 8 ambao unanufaisha zaidi ya kaya 170 katika vijiji vinne vya jirani ambavyo vinategemea sana shughuli za kilimo. 


Alefuddin Muhammadi ni mkulima wa Pazhak anasema sasa mambo yamebadilika.  “Kabla ya kurekebishwa mfereji kulikuwa na matatizo mengi sana, tulikuwa tunafungulia maji usiku na baada ya saa 7 mpaka 8 unakuta maji bado hayajafika kwenye ardhi yetu. Tumekumbana na changamoto nyingi sana, hata ukame tulipata, maji yalikuwa yapite vijiji vingi sana kabla ya kutufikia sisi, hii inamaanisha kuwa hatukuweza kupata maji ya kutosha ardhi yetu. Sasa mfereji huu umeleta mabadiliko mazuri sana kwenye maisha yetu, awali ardhi yetu ilikuwa kame, sasa yote inamwagiliwa.”


Mkulima Hazrat Mohammad ambaye ni naibu kiongozi wa Kijiji cha Pazhak 
anaunga mkono kauli ya Alefuddin, kuhusu kukosa maji kwa wakati na kwamba sasa hawana migogoro tena.   “Watu hawana malalamiko tena juu ya usambazaji wa maji, na kila mtu anaona anapata maji kiwango anacho stahili. Hapo awali watu walikuwa wanapanda zao la ngano sababu linaota hata kwa maji kidogo lakini sasa Pazhak tunapanda Mahindi, viazi na maharage. Upotevu wa maji pia umepungua kwa asilimia 25. Kijiji kingine mavuno ya mazao yao yameongezeka kwa zaidi ya asilimia miamoja sababu ya mfereji huu. Kiwango cha fedha anachopata mkulima sasa kitaongezeka mara mbili zaidi.” 


Ukarabati wa mfereji huo wa umwagiliaji sasa unawezesha usambazaji sawa wa maji, kupunguza upotevu wa maji, ardhi imekuwa na rutuba na yote inatumika kwa kilimo, wakulima wanalima mazao mchanganyiko nakujipatia kipato kikubwa zaidi kama anavyosema msimamizi wa mradi wa Maji, Naser Waziri
“Mradi huu umeboresha ustawi wa maisha ya watu. Takriban asilimia 30 ya wanavijiji wameona mabadiliko kutokana na mradi huu, na mazao yameongezeka kwa asilimia 30 mpaka 35. Wakulimwa ilibidi wakae makundi ya watu 30 mpaka 40 na kusafisha mfereji ule wa zamani. Lakini sasa tangu urekebishwe maji yanatiririka vizuri na uchafu haukwamishi maji kutembea kwenye mfereji kwahiyo hakuna tena haja ya wakulima kukusanyika pamoja kwa ajili ya kufanyia usafi mfereji na hii imeoneza matokeo chanya kwenye kilimo chao.”


Hadi sasa Benki ya Dunia imetoa ufadhili wa zaidi ya Dola za Kimarekani Bilioni 5.3 kwa miradi ya Maendeleo. ARTF imekusanya jumla ya Dola Bilioni 12.9 zote zikilenga kulijenga upya taifa la Afghanistan. 

 

Audio Credit
Assumpta Massoi/Leah Mushi
Sauti
4'41"
Photo Credit
UNAMA/Eric Kanalstein