Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Israel na Palestina zipate suluhu maana watoto wanateseka: UNICEF

Israel na Palestina zipate suluhu maana watoto wanateseka: UNICEF

Pakua

Mashambulizi ya mara kwa mara katika Ukanda wa Gaza, Palestina yamesababisha mama wa watoto watatu wa kiume kuwaza na kuwazua kuhusu mustakabli wa watoto hao ambao kila uchao ndoto zao zinakumbwa na sintofahamu. Kulikoni? Ahimidiwe Olotu anafafanua zaidi.

Eneo ni Ukanda wa Gaza huko Palestina, taswira ni magofu ya nyumba yaliyosalia baada ya kuangushiwa makombora. Woroud, mama wa watoto watatu akiondoa vumbi kwenye nyumba yao anasema, “mara ya kwamba mashambulizi yalipoanza wote walikuwa wamelala. Shambulizi la pili, umeme kwenye jengo letu ulikatika. Shambulizi la tatu tukadhani wanalenga nyumba yetu. Nyumba ilitikisika, vioo vikaanguka. Tukahisi kama masikio yameziba."


Woroud mwenye umri wa miaka 35 anasema walihisi kombora linalofuatia litawashambulia wao. Hata hivyo anasema waliposikia jirani yao anawaita ndipo akafahamu kuwa jengo lao halijapigwa bomu.
Salama yao ilikuwa ni jengo la shule inayoendeshwa na shirika la Umoja wa Mataifa la usaidizi kwa wakimbizi wa kipalestina UNRWA. Hata hivyo watoto wamekumbwa na tatizo akisema, "Watoto wangu wanakumbwa na kiwewe na akili kila wanaposikia sauti yoyote. Wanaziba masikio yao na kuonesha hofu kubwa. Fikra zangu sasa ni maisha yao ya baadaye. Hakuna mtu anayeweza kuwapatia hakikisho la baadaye hapa tulipo."


Hofu ya Woroud na wazazi wengine imefanya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto,  UNICEF litoe wito wa kupatikana kwa suluhu ya kudumu ya kisiasa kati ya Israel na Palestina kwa mustakabali bora wa watoto.
 

Audio Duration
1'48"
Photo Credit
© UNICEF/Eyad El Baba