Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miaka 10 ya Uhuru Bado Sudan Kusini inahitaji msaada : Nicholas Haysom

Miaka 10 ya Uhuru Bado Sudan Kusini inahitaji msaada : Nicholas Haysom

Pakua

Taifa changa zaidi duniani Sudan Kusini linaenda kutimiza muongo mmoja tangu kupata uhuru wake lakini Umoja wa Mataifa unasema bado kuna kazi kubwa ya kufanya kwani baadhi ya makubaliano hayatekelezwa, watu wenye nia ovu wanaendelea kuwatesa raia na wafanyakazi wa mashirika ya misaada nao wanavamiwa na kuuawa. 
Julai 9, mwaka 2011 Sudan Kusini ilijipatia uhuru wake baada ya kujitenga kutoka Sudan, na hivyo kuwa taifa changa zaidi duniani.  
 
Sasa taifa hilo linatimiza miaka 10 na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika kikao chake limetaka kufahamu kutoka kwa Nicholas Haysom Mwakilishi  Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja huo nchini Sudan  hali ikoje? 
 
Haysom ambaye pia ni Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini  Sudan Kusini katika taarifa yake anasema misaada ya kimataifa imesalia kuwa kitu muhimu wakati huu wanajitahidi kupata amani, usalama na ustawi kwa raia wake lakini mwendo ni kama kinyonga. 
 
“Utekelezaji wa makubaliano yaliyofufuliwa kwa ujumla unaenda polepole. Uundaji wa Bunge bado haujamilika, Katiba ya Baraza na uteuzi wa Spika wa Bunge navyo vinasubiri. UNIMISS inaendelea kuihamasisha serikali kukamilisha michakato na huku tukihakikisha kuna uwakilishi wa kutosha wa wanawake na vijana. ’’  
 
Haysom pia amezungumzia hali ya usalama ambayo imekuwa ikisuasua baada ya watu wenye silaha kuwavamia wanavijiji na kufanya uharibifu, katika kipindi cha mwaka huu wa 2021 na asilimia 80 ya walioumia ni wanajamii lakini kubwa linalomtia shaka ni mauaji ya watumishi wa mashirika ya kimataifa na uporaji wa misaada ya kibinadamu. 
 
“Mauaji ya kikatili na ya kibaguzi ya watoa misaada ni yakusikitisha. Kwanza ninatambua jukumu la serikali ni kulinda raia wake na wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu. wakati huo huo UNIMISS inatambua mchango wake muhimu kuweka mazingira salama kwa washirika wake na wafanyakazi wa misaada ya kibadamu. Ujumbe unaendelea kuongoza katika kukuza na kutetea hali ya usalama ambayo inaruhusu kuendelea kwa utoaji wa huduma za kuokoa maisha. ’’   
 
Kwa mujibu wa ripoti ya katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Sudan Kusini inakabiliwa uhaba wa chakula pamoja na utapiamlo ambapo zaidi ya asilimia 60 ya wananchi wake hawana uhakika wa chakula. 
 

Audio Credit
Assumpta Massoi/Leah Mushi
Audio Duration
2'34"
Photo Credit
UN Photo/Isaac Billy