Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wanafaa kuwa moja ya Vipaumbele Muhimu kwenye Mizozo :Gamba

Watoto wanafaa kuwa moja ya Vipaumbele Muhimu kwenye Mizozo :Gamba

Pakua

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya watoto kwenye mizozo ya kivita Virginia Gamba amesema inasikitisha kuona ripoti ya mwaka kuhusu watoto na mizozo ya silaha inachapishwa katika kipindi ambacho bado kuna mateso makali kwa watoto katika maeneo mbalimbali ulimwenguni.

Anachosema Bi Gamba, kama ilivyo kwa watoto wengine katika maeneo yenye mizozo, kinadhihirika katika maisha ya mtoto Gabazech wa nchini Ethiopia mwenye wa umri wa miaka 8. Anaishi katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Baide nchini mwake Ethiopia. Mizozo sugu ya ardhi, imewatawanya watu 100,000 kutoka katika maeneo yao. 
“Njiani kuja hapa, nilibebwa. Nilikuwa nimechoka. Kulikuwa na watu wengi ambao walipoteza nyumba zao katika moto kama sisi.” Anaeleza mtoto huyu aliyeshuhudia madhila makubwa akiwa na umri mdogo. 
Mtoto Gabezech anasema anapenda kujifunza. “Nilikuwa chekechea. Tulijifunza kwa kuimba, “A, B, C, D, X, Y, Y. Hivyo ndivyo nilivyokuwa ninasoma. Lakini sasa siendi shule.” 
Akiwasilisha Ripoti ya Mwaka ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Watoto na Migogoro ya Silaha, Bi Virginia Gamba amesema, " ni jambo la kusikitisha kujua kwamba ripoti hii inachapishwa wakati wa mateso makali kwa watoto. Watoto hawawezi kuwa kipaumbele cha mwisho cha ajenda ya kimataifa wala kikundi cha watu wanaolindwa kidogo mno duniani.” 
Kwa hivyo Bi Gamba anatoa wito akisema, “tunahitaji kuwapa watoto njia mbadala wa vurugu na unyanyasaji.” 
Ripoti hiyo inaonesha kuwa mwaka wa 2020, hali ya watoto katika mizozo ya silaha ilikuwa na idadi kubwa ya ukiukwaji mkubwa wa haki. Umoja wa Mataifa ulithibitisha ukiukwaji 23,946 katika mwaka huo wa 2020. Ukiukaji wa haki uliathiri watoto 19,379 (wavulana 14,097, wasichana 4,993, na 289 hawajulikani jinsia zao).  
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, idadi kubwa zaidi ya ukiukwaji mkubwa wa haki ulithibitishwa nchini Afghanistan, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo - DRC, Somalia, Syria na Yemen. 
 

Audio Credit
Assumpta Massoi/Lucy Igogo
Audio Duration
2'40"
Photo Credit
© UNHCR/Jordi Matas