Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tulinde Mazingira tutapata manufaa hasa kwenye kilimo

Tulinde Mazingira tutapata manufaa hasa kwenye kilimo

Pakua

“Baiyonuai inapungua, hewa ya ukaa inazidi kuongezeka, na uchafuzi wa hewa unaweza kuonekana kila sehemu kuanzia visiwani hadi milimani, ni lazima tufanye maamuzi ya kuwa na uhusiano mwema na mazingira yetu.”

 Ni ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alioutoa leo katika siku ya kimataifa ya kupambana na kuenea kwa jangwa na ukame duniani.
 
Guterres amesema iwapo jamii zitachukua jukumu la kurekebisha ardhi iliyomomonyoka na kukauka, basi hewa ya ukaa itaondoka angani na jamii zilizoathirika zitapata hali nzuri ya hewa na hii italeta ongezeko la dola za Kimarekani trilioni 1.4 kutoka kwenye uzalishaji wa kilimo kila mwaka. 
 
 "Urejeshaji wa ardhi katika hali nzuri ni jambo rahisi, lisilo na gharama na linaweza kufanywa na kila mtu. Jambo hili ni la kidemokrasia na la kusaidia kuongeza chachu ya kufikiwa kwa Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs.” 
  
Guterres amesisitiza kuwa ustawi wa watu Bilioni 3.2 unadhoofishwa kutokana na uharibifu unaofanywa na shughuli za kibinadamu ambazo zinachangia kuongezeka kwa mmomonyoko wa udongo na hata kuweka upenyo wa kushamiri kwa magonjwa ya kuambukiza kama vile COVID-19
 
Katibu Mkuu amekumbusha kuwa mwaka huu ndio mwanzo wa muongo wa kurejesha baiyonua hivyo amesihi siku ya leo itumike kufanya ardhi yenye afya kuwa kitovu cha mipango ya kitaifa na kimataifa. 

Audio Credit
Assumpta /Guterres
Audio Duration
1'26"
Photo Credit
Unsplash/Johannes Plenio