Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatma ya Niger mashakani kwani watoto asilimia 99 hawajui kusoma na kuandika

Hatma ya Niger mashakani kwani watoto asilimia 99 hawajui kusoma na kuandika

Pakua

Ikiwa leo ni siku ya mtoto wa Afrika, ndoto za kutimiza ajenda ya bara hilo ya mwaka 2040 ya kuwa na bara la Afrika linalomfaa mtoto wa Afrika ikiwemo katika suala la kupata elimu, kwa Niger huenda lisitimie kwani asilimia 99 ya watoto wenye umri wa miaka 10 ni wajinga wa kutokujua kusoma na kuandika kulikoni? Flora Nducha anatupasha zaidi 
Mwanafunzi Salif Namaka akisema ana imani na usemi usemao elimu ndio msingi wa maendeleo na elimu ndio inayompa mtoto maafira ya kukabili mustkabali autakao lakini anahoji je itawezekana kwa taila lake la Niger? 
Kwa mujibu wa Benki ya Dunia asilimia 99 ya watoto wa umri wa miaka 10 ni maamuma wa kutokujua kusoma na kuandika nchini humo wakiwa hawajui A wala B, na zaidi ya nusu ya watoto wenye  umri wa miaka 7 na 12 hawako shuleni kwa sababu ya ukosefu  wa rasilimali na mahali ya kusomea.

Mohamed Garba ni mwalimu katika moja ya shule nchini humo na anasema, “Lengo letu ni kuwaelimisha Watoto lakini kwa bahati mbaya shule ni kama imetelekezwa , tuna idadi kubwa ya wanafunzi madarasani, wanafika 100 kwa darasa na unaona mwalimu hawezi kukidhi mahitaji ya watoto wote. Bila kuwa na miundombinu ya kutosha hatuwezi kutimiza malengo yetu ya elimu.” 

Kauli hiyo inaungwa mkono na mwalimu Mariam Hamadou akisema hawana rasilimali zinazohitajika ikiwemo vitabu vya kufundishia na vifaa vingine muhimu. 

Wanafunzi hupaswa kumaliza miaka 12 shuleni lakini asilimia kubwa ya wanafunzi Niger hukaa shuleni wastani wa miaka 5.3 pekee, sababu kubwa ikiwa ni vita, mila na desturi na kubwa zaidi kutokuwa na rasilimali. 

Kwa kutambua umuhimu wa kutimiza lengo la elimu nchini humo sasa Benki ya dunia imeanzisha mradi ujulikanao kama “Kuboresha usomaji kwa ajili ya matokeo chanja katika elimu “ au LIRE. 

Mradi huu unasaidia juhudi za serikali kuimarisha mfumo wa elimu Niger, lakini pia utaboresha mazingira ya kazi kwa waalimu na hasa kwenye maeneo yenye mizozo ili wavulana na wasichana kama mwanafunzi Samira Adamou ambaye ni binti pekee kwenye familia yake waweze kupata elimu bora na kufikia uwezo wao.

Akiwa na matumaini makubwa  Samira anasema,  "ni wajibu wangu kujikita na masomo kwa sababu nina kaka mmoja tu mkubwa na tayari anafanya kazi, mdogo wangu anatakiwa kufuata nyayo zangu na ninatumai kuwafanya wazazi wangu wahisi fahari kubwa kwa kusoma kwa bidii kwani wananitumainia” 
 

Audio Credit
Assumpta Massoi/Flora Nducha
Audio Duration
2'37"
Photo Credit
World Bank/Arne Hoel