Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Apu za utumaji fedha kwa njia ya simu ni muarobaini wa kupunguza umaskini- Dkt. Minja

Apu za utumaji fedha kwa njia ya simu ni muarobaini wa kupunguza umaskini- Dkt. Minja

Pakua

Hoja ya IFAD ya athari za COVID-19 katika utumaji wa fedha kifamilia na nafasi ya teknolojia ya simu za mkononi kufanikisha utumaji wa fedha inaungwa mkono na Dkt. Frank Minja mkazi wa Atlanta Georgia hapa Marekani.

Dkt. Minja ni Rais wa Baraza la Watanzania waishio Marekani (DICOTA) na ni miongoni mwa watu wanaotuma fedha nyumbani akielezea kwanza umuhimu wa siku ya leo akisema, “zile fedha ambazo tunazituma zinamchango mkubwa sana sio tu kwa familia hata kwa jamii nzima kwa ujumla kwa maana ya kiuchumi.” 

Kuhusu janga la COVID-19 na utumaji fedha Dkt. Minja anasema, “kipindi hiki cha janga la corona au COVID-19 , mahitaji pia yameongezeka katika jamii kwa ujumla na pia imekuwa changamoto katika njia mbalimbali za kutuma pesa nyumbani , lakini tunashukuru sana kuna teknolojia mpya , apu ambazo watu wanaweza kutuma pesa  pamoja na mifumo mingine mbalimbali ya kiteknolojia ambayo imerahisisha sana uwezo wetu wa kuweza kutuma pesa nyumbani. Lakini pia najua kwa sababu watu wengi labda wamepoteza ajira zao na pia wametetereka kiuchumi  kwa sababu ya janga hili la COVID-19, ule utumaji pesa umekuwa kidogo umepungua , lakini pamoja na hayo wengi sana wamejitahidi kutuma pesa nyumbani ili kuweza kukidhi mahitaji ya familia zetu kule nyumbani.” 

Dkt. Minja akatoa wito wake katika suala la utumaji fedha akisema, "najua kabisa kadri gharama za kutuma pesa zitakavyozidi kupungua na mifumo itakavyoimarika katikia kutuma fedha nyumbani basi sisi ambao tuko kwenye diaspora tutahamasika Zaidi kutuma pesa nyumbani ili kusaidia ndugu jamaa na marafiki na pia kuchangia katikia uchumi katika nchi zetu huko Afrika Mashariki."

Audio Duration
1'48"
Photo Credit
UN News/Nam Cho