Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Fikisheni teknolojia ya simu kiganjani vijijini nao wanufaike na utumaji fedha kimtandao- IFAD

Fikisheni teknolojia ya simu kiganjani vijijini nao wanufaike na utumaji fedha kimtandao- IFAD

Pakua

Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa maendeleo ya kilimo, IFAD umesema ingawa kiwango cha wahamiaji kutuma fedha nyumbani kimtandao  wakati wa janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 mwaka 2020 kiliongezeka, bado kaya za vijijini zilishindwa kunufaika vyema na utumaji huo kutokana na kukosa miundombinu ya kidijitali ya kupokea fedha hizo. IFAD imesema hayo ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya familia kutumiana fedha kama anavyosimulia Leah Mushi. 
Simulizi yangu inaanzia kijijini nchini Nepal, kwa familia ya Pushpa Raut wakiwa wanaendelea na shughuli za  kila siku huku tegemeo la fedha za kujikimu ni kutoka kwa  mumewe afanyaye kazi ughaibuni. "Mume wangu amekuwa anafanya kazi nje ya nchi kwa miaka 10 sasa. Hivi sasa yuko Dubai akifanya kazi zinazohusiana na ushonaji.” 

Mumewe ni miongoni mwa wafanyakazi wahamiaji milioni 200 ambao hutuma fedha nyumbani, fedha zitumiwazo kwa mahitaji ya chakula, karo za shule na afya. 

Ilikadiriwa kuwa utumaji fedha ungalipungua kwa sababu ya  janga la COVID-19, kutokana na vikwazo vya kutembea na kufungwa kwa benki,  lakini kiwango hicho kilipungua kwa asilimia 1.6 pekee hadi kufikia dola bilioni 540, hali inayoonesha umuhimu wa utumaji fedha.

Maria Bibiana Carreara, wa kampuni ya Bancolumbia itumayo fedha kwa njia ya mtandao anasema, “COVID-19 imeonesha kuwa ijapokuwa wacolumbia walipata shida za kiuchumi, waliendelea kutuma fedha kusaidia familia zao.” 
IFAD inasema utumaji fedha kimtandao uligeuka kimbilio na kiwango cha fedha zilizotumwa kwa simu za kiganjani pekee kiliongezeka kwa asilimia 65 na kufikia dola bilioni 12.7 mwaka 2020 pekee. 

Hata hivyo ukosefu wa intaneti ya uhakika vijijini unafanya familia za vijijini siyo tu zishindwe kupokea fedha kiganjani bali pia ziingie gharama kubwa kupata huduma hiyo. 

Ni kwa mantiki hiyo Meike Van Ginneken afisa kutoka IFAD anasema “katika dunia ya uchumi wa kisasa, utumaji fedha kimtandao ndio taswira ya utandawazi na jamii ya kimataifa inapaswa kushirikiana kuifanya huduma hiyo siyo tu iwe rahisi bali pia ifikie mamilioni ya familia na jamii ambako wanaishi.” 

Takwimu zinaonesha kuwa mtu 1 kati ya 7 duniani anategemea fedha zinazotumwa kutoka kwa jamaa hivyo IFAD inasema kurahisisha huduma hiyo ya kiteknolojia kunamaanisha kuwatoa mamilioni ya watu kutoka katika lindi la umaskini. 
 

Audio Credit
Assumpta Massoi/Leah Mushi
Audio Duration
2'15"
Photo Credit
IOM/ Yasir Elbakri