Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa wafundisha wanajeshi wa Lebanon mbinu za medani na usimamizi

Umoja wa Mataifa wafundisha wanajeshi wa Lebanon mbinu za medani na usimamizi

Pakua

Huko nchini Lebanon, ujumbe wa kikosi cha mpito cha Umoja wa Mataifa nchini Lebanon, UNIFIL, umefanya mazoezi ya siku tano pamoja na vikosi vya usalama vya taifa hilo, LAF kama sehemu ya kujengea uwezo jeshi hilo la kitaifa kwa ajli ya kuimarisha amani na usalama. Ahimidiwe Olotu na maelezo zaidi.  

Eneo la Naqoura nchini Lebanon, makao makuu ya kikosi cha mpito cha Umoja wa Mataifa, UNIFIL,  walinda amani wakifanya mazoezi kwa kutumia silaha nzito za moto, zikiwemo bunduki, silaha ndogo na vifaru.  

Katika zoezi hili, walinda amani wanaonekana wakimbeba majeruhi, na hapa wanapata stadi za kuokoana pindi kuna shambulizi.  

Likipatiwa jina Steel Storm, zoezi hili la siku tano limejumuisha walinda amani kutoka Ufaransa, Finland, Ghana, Korea Kusini, Malaysia, Poland, Ireland, Italia, India, Indonesia, Nepal na Hispania.  

Kanali Enrique Biosca Ponce ni Naibu Mnadhimu Mkuu UNIFIL na anasema,“kwa hiyo zoezi hili ni muhimu sana kwa kweli kwa sababu tunatoa mafunzo siyo tu kwa kutumia silaha halisi, bali pia uratibu wa vifaa na jeshi la Lebanon na kuwajengea imani wanajeshi katika kutumia silaha na kuratibiana na wadau wao.”  

Na zaidi ya yote Kanali Ponce anasema, “kwa hiyo zoezi hili linahusisha siku tano za kufyatua risasi halisi. Kila siku ina ratiba ngumu kwa vikosi na kombania ambazo zinatumia risasi na mabomu halisi kuzingatia kanuni za usalama kuhakikisha zoezi linakuwa salama.”  

Zoezi aina hii hufanyika mara mbili kwa mwaka, kwa mujibu wa azimio namba 1701 [Moja Saba Sifuri Moja] la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ili kujengea uwezo jeshi la Lebanon ambalo lina wajibu wa kusimamia ulinzi na utulivu kusini mwa nchi hiyo kwenye eneo la mvutano na Israel.  

Mwaka jana, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na kukaribisha kupanuliwa kwa wigo wa ushirikiano kati ya UNIFIL na LAF, lilitoa wito wa kuimarishwa zaidi kwa ushirikiano wa sasa.  

Katika mwaka hu wa 2020, kulikuwepo na shughuli 1,070 za pamoja kati ya vikosi hivyo ikiwemo mazoezi, mafunzo na warsha ambavyo vyote vilifanyika nchi kavu na baharini.  

UNIFIL ilianzishwa tarehe 19 mwezi Machi mwaka 1978 pamoja na mambo mengine kuthibitisha kuondoka kwa vikosi vya Israel kutoka eneo la kusini mwa Lebanon.  

Audio Credit
Assumpta Massoi/Ahimidiwe Olotu
Audio Duration
2'25"
Photo Credit
UN /Pasqual Gorriz