Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yatoa fedha kila mwezi kwa kaya masikini Ethiopia

UNICEF yatoa fedha kila mwezi kwa kaya masikini Ethiopia

Pakua

Nchini Ethiopia mpango wa kusaidia kaya maskini kwa kuzipatia fedha, sasa unaongezwa kiwango cha fedha kutoka dola 13 kwa mwezi hadi dola 21 kwa mwezi baada ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF na wadau kuingia makubaliano ya kusaidia serikali katika mpango huo kwa miezi sita ijayo. Assumpta Massoi na maelezo zaidi. 


(Taarifa ya Assumpta Massoi) 
Katika viunga vya mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa ndani ya makazi duni tunakutana na Hannah Zerihun, mama wa watoto wawili. 

Yeye ana ulemavu wa mkono mmoja na mguu, hali ambayo inafanya ashindwe kuajiriwa au kujiajiri na kupata kipato kwa ajili ya familia yake.  
Ingawa hapa nyumbani kwake analazimika kufanya kazi zikiwemo za usafi na mapishi kwa ajili ya watoto wake. 
Hannah anasema, “baba wa watoto wangu aliniacha mara tu baada ya kupata watoto wawili. Katu hakunisaidia kifedha. mpango wa kunusuru kaya unanisaidia.” 


Makali ya maisha na hali ya ulemavu vilisabababisha ajumuishwe kwenye mpango wa serikali wa kunusuru kaya za maskini mijini ambapo hupatiwa dola 13 kila mwezi kupitia akaunti ya benki.  
Na sasa kutokana na COVID-19, wanapatiwa fedha za mkupuo za miezi mitatu. 
Na zaidi ya yote, serikali ya Ethiopia imeongeza mgao wa fedha hadi dola 21 kwa mwezi ambapo UNICEF na wadau watajazia dola 10 ya nyongeza hiyo ya mwezi kwa kila mtu kwa kipindi cha miezi sita ijayo. 


UNICEF pia imewezesha serikali kuwa na wafanyakazi wa kijamii ambao wataunganisha watu kama Hannah na huduma nyingine za kijamii ikiwemo bima ya afya kupitia mfuko wa bima ya jamii sambamba na kuwapatia ushauri nasaha wakati wowote wanapohitaji. 
 

Audio Credit
Leah Mushi/ Assumpta Massoi
Audio Duration
2'4"
Photo Credit
Picha: IOM Ethiopia