Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Corona yachangia ongezeko la ajira za utotoni

Corona yachangia ongezeko la ajira za utotoni

Pakua

Kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miongo miwili, ajira za utotoni zimeongezeka na kufikia watoto milioni 160 na huenda takwimu hizo zikapanda kwa mwaka ujao wa 2022 iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa kuwalinda watoto.

Taarifa hii ipo kwenye ripoti iliyotolewa leo na Mashirika mawili ya umoja wa mataifa lile la kushughulikia watoto UNICEF na la ajira ILO mjini Geneva Uswisi.  Tuungane na Jason Nyakundi kwa ufafanuzi zaidi. 

(Taarifa ya Jason Nyakundi)
Ripoti hiyo ya ILO na UNICEF imeeleza namna familia zilivyofanya maamuzi magumu kwa watoto wao kuingia kwenye ajira ilihali wana umri mdogo na kinacho huzunisha zaidi ni kuwa, watoto kati ya miaka mitano mpaka 11 ndio wengi zaidi ukilinganisha na watoto wenye umri kati ya miaka 11 mpaka 17.

Pia imeonya watoto milioni 9 wapo kwenye hatari ya kuingia kwenye ajira ifikapo mwaka 2022 kutokana na athari za janga la Corona na iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa idadi hiyo inaweza kuongezeka nakufikia milioni 46.

“Tunapoteza muelekeo katika vita hii ya kukomesha ajira za utotoni” amesema mkurugenzi mtendaji wa UNICEF Henrietta Fore, “sasa ukiwa ni mwaka wa pili kujifungia ndani kupambana na corona, shule kufungwa uchumi kuathirika na kushuka kwa bajeti za kitaifa, familia zimefanya maamuzi magumu. Tunazishauri serikali na benki za maendeleo kuwekeza katika programu zitakazo watoa watoto kwenye ajira na kuwarejesha shuleni, na pia kuzisadia familia ili ziweke kuepuka kufanya uamuzi magumu wa kuruhusu watoto wadogo waingie kwenye ajira”

Ripoti imebainisha katika ukanda wa jangwa la Sahara, ndani ya miaka minne watoto milioni 16.6 wameingia kwenye ajira na wengi wao kutoka vijijini. Mkurugenzi mkuu ILO Guy Ruder amesema ni dhahiri tumeshindwa kuwalinda watoto. 

Takwimu hizi zinatuamsha kutoka kwenye limbi la usingizi, hatuwezi kuacha kufanya kitu wakati kizazi kipya kipo hatarini. Tukifanya ulinzi wa pamoja tutasaidia familia kuhakikisha watoto wao wanabaki shuleni hata wanapopatwa na hali mbayá ya kiuchumi. Kuongeza uwekezaji vijijini na kwenye masuala ya kilimo, huu ni wakati wa kuhakikisha tunavunja mzunguko wa umasikini na ajira za utotoni. 

Asilimia 70 ya watoto wameajiriwa kwenye sekta ya kilimo ikifuatiwa na huduma ambayo ni asilimia 20, na asilimia 10 iliyobaki ni kwenye viwanda. 

 

Audio Credit
Leah Mushi/Jason Nyakundi
Audio Duration
2'18"
Photo Credit
OCHA/Gemma Connell