Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tanzania yawa Makamu wa Rais UNGA76 na mjumbe wa ECOSOC

Tanzania yawa Makamu wa Rais UNGA76 na mjumbe wa ECOSOC

Pakua

Tanzania imechaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA utakaoanza tarehe mosi mwezi Septemba mwaka huu. 

Kwa mujibu wa Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Profesa Kennedy Gastorn, uchaguzi huo umefanywa na nchi wanachama, siku ya Jumatatu Mei 7, Tanzania ikiwa ni miongoni mwa makamu marais 9 wa mkutano huo utakaoongozwa na Rais wa mkutano huo wa 76 Abdulla Shahidi kutoka Maldives. 

Uchaguzi huo pia ulifanyika kumchagua Bwana Shahidi ambaye alimshinda mpinzani wake kutoka Afghanistan. 

Katika uchaguzi huo, Tanzania ilipita bila kupingwa na mara ya mwisho Tanzania kuwa Makamu wa Rais ni 1991. Tanzania ilishakuwa Rais mara moja tu katika mkutano wa 34 wa UNGA mwaka 1979 wakati wa uwakilishi wa Balozi Dkt. Salim Ahmed Salim.  

Majukumu ya Makamu wa Rais 

Majukumu ya Makamu wa Rais ni kusaidiana na Rais katika kuratibu na kusimamamia shughuli za mijadala ya UNGA na kamati zake katika kutunga maazimio. 

Baraza kuu La Umoja wa Mataifa ndio chombo kikuu cha kutunga sera na sheria chenye uwakilishi wa nchi zote wanachama.  

Tanzania yachaguliwa mjumbe wa ECOSOC 

Balozi Profesa Gastorn amesema katika uchaguzi huu pia, Tanzania imeshinda kuwa kati ya wanachama 54 wanaounda Baraza la Kiuchumi na Kijamii la Umoja wa Mataifa (Economic and Social Council (ECOSOC)) kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia tarehe 1 mwezi Januari mwaka 2022. 

Tanzania ilipata kura 182 kati ya 186 zilizopigwa.  

“Hii ni mara ya tano kwa Tanzania kushika nafasi hii muhimu na mara ya mwisho ilikuwa 2004-2006. Mara nyingine ilikuwa ni 1966-69; 1978-1980; na 1994-1996. ECOSOC ndio chombo kinachohusika na miradi ya maendeleo ya kiuchumi ya Umoja wa Mataifa hasa katika kutekeleza malengo ya maendeleo endelevu ya 2030, na pia husimamia mashirika yaliyo chini ya Umoja wa Mataifa kama UNDP, UNFPA, UNICEF nk,” amefafanua Balozi Gastorn. ECOSOC pia huratibu mikutano na makongamano ya Umoja wa Mataifa.  

Maana yake kwa Tanzania 

Akichambua zaidi fursa hizo, Mwakilishi huyo wa kudumu wa Tanzania amesema, ushiriki wa Tanzania katika uongozi wa vyombo vya Umoja wa Mataifa unaipa nchi nafasi nzuri kutekeleza sera yake ya mambo ya nje na pia kuchangia utekelezaji wa majukumu yake kama mwanachama wa Umoja wa Mataifa.  

“Mfano, miradi yote ya kiuchumi huratibiwa na ECOSOC na hivyo Tanzania inaweza kutumia ushiriki na ushawishi wake ndani ya chombo hiki ili kuboersha mazingira ya kiuchumi kulingana na sera yake ya diplomasia ya uchumi chini ya utawala imara wa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kuchaguliwa kwake pia ni ishara ya kuaminika katika medani za kimataifa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa.” Amesema Balozi Gastorn. 

Audio Credit
Leah Mushi/Balozi Gastorn
Audio Duration
1'38"
Photo Credit
UN /Manuel Elias