Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maambukizi ya VVU Tanzania yamepungua kwa kiasi kikubwa - Rais Samia

Maambukizi ya VVU Tanzania yamepungua kwa kiasi kikubwa - Rais Samia

Pakua

Tanzania imesema inaunga mkono mshikamano wa kimataifa wa kutokomeza Ukimwi duniani, kauli iliyotolewa leo na Rais wa taifa hilo Samia Suluhu Hassan wakati akihutubia mkutano wa ngazi ya juu wa Baraza Kuu la  Umoja wa Mataifa kuhusu UKIMWI ulioanza leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa kwa njia ya mtandao na ukumbini. Assumpta Massoi na taarifa zaidi.

Mkutano huo wa siku tatu unatathmini maendeleo yaliyofikiwa duniani katika kupunguza maambukizi ya ugonjwa huo tangu kufanyika kwa mkutano wa ngazi hiyo mwaka 2016. 

Mkutano huu umefunguliwa na Rais wa Baraza Kuu Volkan Bozkir na kuhutubiwa pia na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed ambaye amesema kuwa hatua dhidi ya UKIMWI zimeonesha kile kinachowezekana kufanikiwa iwapo kuna utashi wa kisiasa, mshikamano na sayansi na hivyo  lengo la kutokomeza UKIMWI ifikapo mwaka 2030 linawezekana.

Kisha viongozi mbalimbali wakaanza kutoa tathmini za vita dhidi ya UKIMWI katika nchi zao ambapo Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania akihutubia kwa mara ya kwanza Baraza Kuu kwa njia ya mtandao amesema, “Ukimwi siyo tena hukumu ya kifo nchini Tanzania kama ilivyokuwa miaka 38 iliyopita. Vifo vitokanavyo na Ukimwi vimepungua kutoka elfu 64 kwa mwaka 2010 hadi elfu 32 mwaka 2020. Maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto yamepungua kutoka asilimia 18 mwaka 2010 hadi asilimia 7 mwaka 2020.”

Akasema licha ya mafanikio hayo COVID-19 inaleta mkwamo lakini hakuna janga ambalo linapaswa kupewa rasilimali  zaidi kuliko lingine na, “Badala yake tunapaswa kujifunza kutokana na hatua za kukabili UKIMWI kwa kujenga jamii zenye mnepo na mifumo thabiti ya afya ambayo itakabili changamoto zijazo za kiafya na majanga.”

Mkutano huo umepitisha azimio la kisiasa ambalo pamoja na mambo mengine linalenga kuongeza juhudi za kutokomeza UKIMWI duniani ambapo Rais Samia amesema Tanzania inaunga mkono mshikamano huo wa kimataifa.
 

Audio Credit
Leah Mushi/Assumpta Massoi
Audio Duration
2'6"
Photo Credit
Photo: Sean Kimmons/IRIN