Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tulisikia mitetemo na moto kila mahali na tukakimbia- Manusura wa volkano ya Nyiragongo, DRC

Tulisikia mitetemo na moto kila mahali na tukakimbia- Manusura wa volkano ya Nyiragongo, DRC

Pakua

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR na wadau wengine wanawasaidia watu waliolazimika kuyakimibia makazi yao baada ya mlipuko wa volkano katika Mlima Nyiragongo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC. Wengi walivuka mpaka kwenda nchi jirani ya Rwanda ambako sasa wanapata usaidizi. Taarifa ya Assumpta Massoi inaeleza zaidi.
Huyu ni Joyce, raia kutoka DRC ambaye amekimbilia hapa Rubavu nchini Rwanda akisimulia alichoshuhudia huko kwao jimboni Kivu Kaskazini ambako volkani kutoka mlima Nyiragongo ilianza kulipuka tarehe 22 mwezi uliopita wa Mei.
Video ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR inaonesha misafara ya kuingia Rwanda; iwe ni kwa magari au kwa miguu, kila mtu akibeba kirago alichoweza kuchukua.
Esther, mkimbizi kutoka DRC anasimulia akisema, “tuliona mlipuko wa moto kutoka volkano ya Nyiragongo saa kumi na mbili jioni. Moto ulisambaa, uliua wat una kuharibu mashamba pamoja na nyumba na vijiji. Tulikimbilia Rwanda ili kuokoa maisha yetu.
Baada ya kuingia Rwanda, wakimbizi hawa walisajiliwa ambapo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR pamoja na wadau wanawapatia pia msaada wa chakula na malazi.
Esther bado ana kumbukumbu za kule alikotoka baada ya volkano kulipuka akisema, “mali zetu zote ziliharibiwa vikiwemo vifaa vya nyumbani na vyakula pamoja na nyumba yetu. Mbuzi wetu wote walikufa. Kila kitu tumeacha DRC.”
Kwa sasa angalau faraja ya wakimbizi hawa ni kwamba kuna mahali pa kujihifadhi na mlo ambao unaleta hata tabasamu kwa watoto.
Mara ya mwisho  mlima Nyiragongo kulipuka volkano yake ilikuwa mwaka 2002 ambapo watu zaidi ya 200 walikufa na wengine 100,000 walipoteza makazi yao.
Mlipuko wa mwaka huu umesababisha vifo vya watu 32 na watu 350,000 wanahitaij msaada.
Volkano ya Mlima Nyiragongo inatajwa kuwa miongoni mwa volkano hai na hatari duniani.
 

Audio Credit
Leah Mushi/Assumpta Massoi
Audio Duration
2'21"
Photo Credit
© UNICEF/Jean-Claude Wenga