Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Waasi DRC wavamia kambi za wakimbizi wa ndani na kuua raia 55, UN yapaza sauti

Waasi DRC wavamia kambi za wakimbizi wa ndani na kuua raia 55, UN yapaza sauti

Pakua

Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani vikali mashambulio ya siku ya Jumatatu yaliyofanywa na waasi wa Allied Democratic Forces (ADF) dhidi ya wakimbizi wa ndani huko Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na kusababisha vifo vya raia 55 na wengine wengi wamejeruhiwa. Grace Kaneiya na maelezo zaidi.

Taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa iliyotolewa Jumanne usiku jijini New York, Marekani imesema waasi hao wa ADF walishambulia kambi za wakimbizi wa ndani zilizoko karibu na mji wa Boga jimboni Ituri na  mji wa Tchabi jimboni Kivu Kaskazini na kuua raia hao 55.

Katibu Mkuu ametuma salamu za rambirambi kwa familia za waliouawa kwenye mashambulizi hayo huku akiwatakia ahueni ya haraka majeruhi.

Ametoa wito kwa mamlaka za DRC kuchunguza haraka matukio hayo na kuwafikisha mbele ya sheria wahusika.
  
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO, ulipelekwa kwenye miji hiyo ambako walinda amani wanapatia huduma majeruhi sambamba na kusafirisha wale wanaohitaji huduma zaidi za matibabu.
  
Katibu Mkuu amesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa kupitia mwakilishi wake maalum nchini DRC, utaendelea kusaidia serikali ya DRC na wananchi wake katika juhudi zao za kuleta amani na utulivu mashariki mwa taifa hilo.

Audio Credit
Leah Mushi/Grace Kaneiya
Audio Duration
1'17"
Photo Credit
© UNICEF/Roger LeMoyne