Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa UNIDO umeniondolea Umasikini

Mradi wa UNIDO umeniondolea Umasikini

Mradi wa kuwezesha wanawake nchini Sudan Kusini unaoendeshwa na shirika la Umoja wa Mataifa la maendeleo ya viwanda UNIDO kwa ufadhili wa serikali ya Canada umekuwa mkombozi mkubwa hasa kwa wanawake wavuvi na wakulima nchini mjini Juba nchini humo sio tu kwa kuwawesha kulisha familia zao lakini pia kupambana na umasikini.

John Kibego anafafanua zaidi 

Kwa mujibu wa UNIDO lengo kubwa la mradi huo uliojikita katika masuala ya uvuvi, usindikaji na kilimo ni kutoa fursa za kiuchumi kwa wanawake kwa lengo la kukuza usawa wa kijinsia hususani kwenye sekta ya kilimo na uvuvi, lakini pia kuwajengea uwezo wa kujitegemea wanawake kama Nejwa Siliman anayeishi mjini Juba na wanawawe na fedha anazozipata kwa kuuza Samaki zinamsaidia kuishi na kulea familia yake na kusomesha watoto wake. 

Nenjwa amepata mafunzo yanayoendeshwa na UNIDO ya kuvua Samaki, kuwasindika na kuwauza, anasema 

"Biashara ya kuuza Samaki ni nzuri, kwa kuwekeza kidogo unaweza kutengeneza fedha nyingi zitakazokusaidia na watoto wako, familia yako na masuala ya shule na naishukuru UNIDO kwa kunipa fursa hii." 

Mradi huu wa mafunzo wa UNIDO umemsaidia Nejwa na wanawake wengine kupambana na umasikini kwa kujiongezea kipato kitokanacho na biashara ndogondogo wanazofanya ambacho kinawawezesha kulinda jamii zao na wanufaika wa kwanza ni wanafamilia wa wanawake hawa. Hurria Osman ni mama wa Nejwa 

"Mwanangu alichojifunza hapa kina faida kubwa kwake na kwetu, chochote anachojifunza na kukipata anakileta nyumbani kinatunufaisha sote" 

Nejwa haendesshi biashara ya Samaki peke yake ameamua kujiunga na kina mama wengine na kuanzisha jumuiya ya wanawake wa Kuru-ko Wate na imekuwa raihis kusaidiwa na UNIDO wakiwa kwenye kikundi ambacho mbali ya uvuvi kinasindika na kutengeneza bidhaa mbalimbali za Samaki na kilimo. 

Lucia Sebit mmoja wa wanajumuiyan hiyo anasema "kitu cha muhimu zaidi kwa wanawake hawa ni ujuzi wanaoupta kupitia mafunzo ya UNIDO, na wamejifunza mengi yaliyowawezesha kuwainua kiuchumi na kuwapa ujasiri wa kujitegemea." 

Ingawa walianza wachache sasa jumuiya hiyo ina wanawake wanachama 135, na hii inamaanisha familia na kaya 135 zimefaidika na kubadili maisha yao zikipiga hatua moja mbele kutokomeza umasikini. 

Na hadi kufikia sasa wanawake zaidi ya 400 wamefaidika na mafunzo mbalimbali ynayotolewa na UNIDO mjini Juba.

Audio Credit
Leah Mushi/John Kibego
Photo Credit
UNICEF/Shehzad Noorani