Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashairi yatumika kusongesha SDGs

Mashairi yatumika kusongesha SDGs

Pakua

Kuweka ujumbe wa Malengo ya Maendeleo Endelevu SDGs katika mashairi ni moja ya njia nzuri za kuyaleta karibu malengo hayo karibu na watu, kuyaelewa na kuyafanyia kazi. Hayo ni maneno ya Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Zlatan Millisic alipokuwa akipokea kitabu cha mashairi 17 ya SDGs kilichoandikwa na kijana mtanzania, Aisha Kingu.  Ahimidiwe Olotu na maelezo zaidi.

“Ndugu umaskini, usiangalie kibanda changu. Usigonge kwenye nyumba ya jirani yangu. Kaa mbali, mbali kabisa.” 

Ni Aisha Kingu, akighani shairi la kwanza kati ya mashairi 17 aliyoaandika ili kueneza ujumbe kuhusu Malengo ya Umoja wa Mataifa ya Maendeleo Endelevu SDGs. Aisha anaeleza kilichomsukuma kuandika mashairi haya na kwa nini ameamua kutumia sanaa hii,  akisema, “tukizungumzia maisha ya binadamu, nadhani asilimia kubwa tunagusia maendeleo endelevu. Kwasababu ndani ya maisha ya binadamu kuna vitu ambavyo vinagusa maisha ya binadamu ya kila siku. Kwa hiyo nikasema ni njia gani rahisi ya kufikia watu ili  maendeleo haya yaweze kufanikiwa kwa urahisi, nikaona kwa sababu nimerabirikiwa kipaji cha uandishi, nikaona nikitumia mashairi itakuwa ni njia…siku zote sana ina nguvu. Kwa hiyo ni njia rahisi ya watu kuelewa, kutambua, kuhamasika ni nini wafanye au ni nini kinaweza kufanyika ili tuweze kufika kile ambacho tuna malengo nacho.” 

Na kuhusu ni kwa nini ana imani kuwa mashairi aliyoyaandika yatafikisha ujumbe kirahisi, Aisha Kingu anasema, "nimashairi ambayo yanahamasisha, yanagundua tatizo, yanatoa njia mbadala, yanahamasisha watu wafanye nini ili waweze kutatua lile tatizo. Kwa mfano tuna tatizo la umaskini. Siyo kwamba limeondoka kabisa lakini serikali na hata jamii kwa ujumla tunajitahidi kuanzia familia, taifa, kimataifa tunapambana kwa pamoja ili tuweze kuondoa janga hilo. Kwa hiyo inagusa kwa namna moja au nyingine lakini pia kwa kutumia lugha hii ya sanaa ya maneno, itafanya jamii iweze kuhamasika zaidi na iweze kutafuta njia muafaka zaidi ili kuweza kufanikisha malengo hayo.”  

Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania Zlatan Millisic anaeleza kufurahishwa kwake na ubunifu wa  msichana huyu…anasema, “njia hii ya ushairi ni nzuri sana ya kuyafikisha malengo ya maendeleo endelevu karibu na watu na mashairi haya yamekuja wakati muhimu zaidi, katika miaka 10 ya mwisho kuelekea kuyatimiza malengo ya maendeleo endelevu.”  

Audio Credit
Leah Mushi/Ahimidiwe Olotu
Audio Duration
2'7"
Photo Credit
UN SDGs