Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR lataka msaada zaidi kwa warundi wanaorejea nyumbani Burundi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR lataka msaada zaidi kwa warundi wanaorejea nyumbani Burundi

Pakua

Akihitimisha ziara ya siku mbili nchini Burundi, Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, Filippo Grandi, amepongeza juhudi zilizofanywa kusaidia wakimbizi kupata suluhu ya muda mrefu katika taifa  hilo ambalo ni kiini cha ukanda wa Maziwa Makuu. 

Bwana Grandi amesema katika ukanda ulioghubikwa na mizozo inayosababisha watu kufurushwa makwao, anatiwa moyo kuona juhudi zinazolenga kutafuta suluhu kwa ajili ya wakimbzi hususan warundi.  

Tangu mwaka 2017 karibu warundi wakimbizi 145, 000 wamesaidiwa kurejea nyumbani kwa hiari,  huku zaidi ya 25,000 wakirejea kutoka Rwanda katika miezi ya hivi karibuni.  

Kwa wastani watu 2,000 wanasaidiwa kurejea nyumbani kwa hiari kila wiki kutoka Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Tanzania.  

Grandi amerejelea dhamira ya UNHCR ya kuendelea kusaidia wakimbizi warundi ambao wamefanya uamuzi wa  hiari kurejea nyumbani akisema, “kurejea kwa wakimbizi kunaweka jukumu kubwa kwa serikali hususan kuhakikisha usalama katika maeneo wanakorejea, ujumuishwaji wa wakimbizi ni lazima uhakikishe upatikanaji wa mali na huduma na uwezo wa kukidhi mahitaji binafsi na ya familia, ama sivyo wanaorejea huenda wakafurushwa tena.”  

Wakati wa ziara yake Kamishna Mkuu huyo alikutana na Rais wa Burundni Évariste Ndayishimiye na kuzungumzia umuhimu wa kuendelea kujenga mazingira salama na yenye hadhi kwa ajili ya wakimbizi wanaorejea nyumbani.   

Mnamo mwezi Februari mwaka huu, UNHCR na serikali ya Burundi na wadau walizindua mpango wa pamoja wa kurejea na kujumuishwa tena wakimbizi na kutoa ombi la dola milioni 104.3 kwa jamii ya kimataifa kwa ajili ya kusaidia wanaorejea na jamii wanakorejea.  

Kufikia sasa ni asilimia chini ya 10 tu ya ombi hilo zimekwishatolewa licha ya ongezeko la wakimbizi wanaorejea nyumbani.  

Katika hatu nyingine Kamishna Mkuu amepongeza Burundi kwa ukarimu wake kuendelea kuhifadhi wakimbizi 80,000 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo licha ya changamoto kubwa za kijamii na kiuchumi zinazoikabili nchi hiyo. 

Aidha ametoa wito kwa msaada zaidi kutoka kwa jamii ya kimatiafa kwa ajili ya kuimarisha hali katika kambi wanakohifadhiwa wakimbizi hao.  

Audio Credit
Grace Kaneiya/Assumpta Massoi
Audio Duration
2'7"
Photo Credit
Photo: IOM Burundi / Gustave Munezero