Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi wa Afghanistan waanza kupatiwa kadi za kisasa za utambulisho nchini Pakistani

Wakimbizi wa Afghanistan waanza kupatiwa kadi za kisasa za utambulisho nchini Pakistani

Pakua

Pakistani imezindua kampeni ya kupatia wakimbizi milioni 1.4 wa Afghanistan nchini humo vitambulisho vya kisasa vitakavyowawezesha kupata huduma za msingi.  John Kibego na maelezo zaidi.

Kazi hiyo inayoenda sambamba na kuthibitisha takwimu zao inafanyika baada ya kampeni kama hiyo kufanyika miaka 10 iliyopita nchini humo. 

Utoaji huo wa vitambulisho vipya utaimarisha juhudi za serikali ya Pakistani kwa msaada wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, za kuimarisha ulinzi wa wakimbizi. 

Ikitambulika rasmi kama zoezi la kupata upya nyaraka na kuthibitisha utambulisho, DRIVE, kampeni itafanyika kwa miezi sita na inalenga wakimbizi wa Afghanistan ambao tayari wana kadi za uthibitisho wa usajili. 

Indrika Ratwatte ni Mkurugenzi wa UNHCR kanda ya Asia na Pasikifi na anasema,  “Wakimbizi wa Afghanistani waliosajiliwa hivi sasa ni milioni 1.4 na wamenufaika na mpango wa kipekee wa Pakistani muongo mmoja uliopita pindi walipoandikishwa na kupatiwa kadi ya uthibitisho wa usajili. Leo tunawapatia tena kadi hizo lakini zikiwa za kisasa na chipu ambapo hakitakuwa tu ni kitambulisho bali pia kitabeba taarifa muhimu kama stadi, mahitaji maalum ya mkimbizi.” 

Kadi za kisasa watakazopatiwa wakimbizi kutoka Afghanistani zitakuwa na alama za vidole na macho na zitadumu kwa miaka miwili na kuwawezesha kupata huduma za msingi nchini Pakistani sambamba na kuwawezesha wale wanaotaka baada ye kurejea nyumbani, waweze kufanya hivyo. 

Akifafanua zaidi Bwana Ratwatte amesema, “Takwimu zitatuwezesha kushirikiana kwa karibu na serikali ya Afghanistan kuoanisha kiwango cha stadi na fursa za kujipatia kipato, kazi kwa wakimbizi na kuendeleza urejeaji nyumbani kwa hiari, pindi wakimbizi watakaporejea Afghanistan. Kwa hiyo kuna faida nyingi.” 

Wafanyakazi 600 wakiwemo wa serikali na UNHCR wataendesha kampeni hiyo katika vituo 35 nchini kote na watatumia magari ili kufikia maeneo hata ya ndani huku wakizingatia kanuni za kuepusha maambukizi ya ugonjwa wa Corona au COVID-19

UNHCR inasaka dola milioni 7 kwa mwaka huu wa 2021 ili kufanikisha mpango huo wa DRIVE ikiwemo vifaa vya teknolojia ya kadi za kisasa, na kuweka vituo vya kusajili. 

Audio Credit
Grace Kaneiya/John Kibego
Audio Duration
2'13"
Photo Credit
UNHCR/Andrew McConnell