Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF: Watoto 275 wanajikuta  Mexico kila siku wakisubiri kuingia Marekani

UNICEF: Watoto 275 wanajikuta  Mexico kila siku wakisubiri kuingia Marekani

Pakua

Tangu kuanza kwa mwaka 2021 idadi ya watoto wahamiaji wanaowasili Mexico wakisubiri kuingia nchini Marekani imeongezeka kwa kasi kutoka watoto 380 hadi karibu watoto 3500 amesema mkurugenzi wa kanda ya Amerika Kusini na Caribbea wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF. Flora Nducha na maelezo zaidi. 

Katika makazi ya Kiki Romero Chihuahua Mexico, mamia ya watoto wakiwa katika malazi ya muda yanayosomamiwa na serikali kwa msaada wa UNICEF wengine wakiwa peke yao na wengine na wazazi au walezi wao.  

Kwa mujibu wa Jean Cough mkurugenzi wa kikanda aliyehitimisha Jumatatu ziara yake ya siku 5 nchini Mexico ambako ametembelea sehemu mbalimbali zinazohifadhi watoto wahamiaji na vituo vya mapokezi mpakani mwa Mexico na Marekani, amesema idadi ya watoto wahamiaji inaongezeka kila uchao kwani sasa kwa wastani watoto 275 wahamiaji wanajikuta Mexico katika makazi ya muda ya wahamiaji kila siku baada ya kubainiwa na mamlaka ya nchi hiyo wakisubiri kuingia Marekani au kurejeshwa walikotoka. 

Jean amesema alitiwa uchungu sana kushuhudia madhila yanayowakabili watoto hao wengine wakiwa ni wadogo sana na makazi yote aliyotembelea yalikuwa yamefurika hayana tena uwezo wa kuongeza idadi ya watoto wahamiaji na familia zao. 

UNICEF inasema nchini Mexico katika makazi yote watoto ni karibu asilimia 30 ya wahamiaji wote na nusu yao wanasafiri peke yao bila wazazi ama walezi ikiwa ni idadi kubwa kuwahi kuorodheshwa nchini humo. 

Wengi wa watoto hao wanatokea Honduras, Guatemala, Elsalvador na Mexico yenyewe. 

Mwaka 2020 UNICEF ilikaribisha mabadiliko ya sheria za uhamiaji na ukimbizi Mexico ambazo zinapiga marufuku kuwaweka mahabusu watoto na kutoa kipaumbele cha kuwasaidia. 

Hata hivyo janga la Corona au COVID-19 limeongeza idadi ya watoto waosafiri peke yao na pia idadi ya wahamiaji wanaowasili familia nzima hali ambayo imeleta shinikizo kubwa kwa serikali ya Mexico katika vituo vya msaada .  

Sasa UNICEF inatoa ombi la msaada wa dola milioni 23 ili kupanua makazi ya kuhifadhi wahamiaji hao nchini Mexico ili kuweza kukidhi mahitaji ya familia zenye watoto na watoto wanaosafiri peke yao ikiwemo ya ulinzi, elimu, huduma za maji na usafi, mafunzo, ujuzi, huduma mbadala na kuzuia vitendo vya ukatili. 

Mwaka jana zaidi ya watoto 7,160 walinufaika na msaada wa UNICEF kwa serikali ya Mexico ambao ulijumuisha huduma za ulinzi, kisaikolojia, elimu na malazi. 

Audio Credit
Grace Kaneiya/Flora Nducha
Audio Duration
2'39"