Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Benki ya Dunia na UNICEF wakomboa wanawake kwa malezi ya watoto Burkina Faso

Benki ya Dunia na UNICEF wakomboa wanawake kwa malezi ya watoto Burkina Faso

Pakua

Nchini Burkina Faso, adha ya wazazi wanawake kushindwa kufanya kazi kwa kukosa walezi wa watoto wao imepata jawabu baada ya Benki ya Dunia na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, kuanzisha mradi wa vituo vya kulelea watoto vinavyofuata akina mama maeneo ambako kuna mradi, na hivyo kuwawezesha kupata kipato na wakati huo huo elimu ya malezi kwa watoto wao. Taarifa ya John Kibego inafafanua zaidi. 

(Taarifa ya John Kibego) 

Nats.. 

Katika moja ya vituo vya malezi ya watoto, Odette anawasili na baiskeli akiwa amebeba watoto wake wawili, wa umri wa miaka miwili na mitatu. 

Kituo hiki ni sehemu ya mradi wa Benki ya Dunia na UNICEF wa kuendeleza vijana hasa wa kike na watoto wao kwa kuwapatia vituo ambamo watoto wao watapata malezi bora bila hofu wakati wao wako kazini. 

Vituo hivi vimejengwa kwa mahema kutoka UNICEF na vinahamahama kwenda maeneo ambako wazazi wao wameajiriwa vibarua. 

Odete ni kibarua katika mradi wa mtulinga wa kazi za umma kwenye eneo la Ziniare, mradi ulionzishwa na Benki ya Dunia mwaka 2016 kwa ajili ya kuajiri vijana na hadi sasa umeajiri watu wapatao 46,000 wengi wao wanawake. Dianda Minata ni mmoja wao. 

(Sauti ya Dianda Minata) 

“Kabla ya kujengwa vituo hivi, hali ilikuwa tofauti. Watoto tuliwabeba mgongoni ili tufanye kazi. Mtoto akilia inabidi uache kazi umbembeleze. Maeneo mengine ya kazi yalikuwa ni hatari mno, watoto walikumbana na nyoka na n’ge.” 

Watoto wanaopokelewa hapa ni kuanzia wachanga wenye miezi 0 hadi miaka 6.  

Wafanyakazi ni baadhi ya wanufaika wa miradi ya mitulinga na wanasimamiwa na wakufunzi wa elimu ya awali kutoka wizara ya elimu ya Burkina Faso na hivyo kuwawezesha watoto kupata elimu bora ya awali, huku wazazi nao wakipatiwa mafunzo ya afya ya watoto wao, mathalani mfululizo wa chanjo. Bi.  Minata ameona mafanikio kwa mtoto wake.. 

(Sauti ya Dianda Minata) 

“Hata nyumbani mtoto anakuwa na tabia kama bado yuko kituoni.  Watoto ambao mara kwa mara wanaugua Malaria, Kipindupindu, na magonjwa mengine yanayohusiana na ukosefu wa usafi, hawajaugua tena tangu waanze kwenda kwenye vituo hivyo.” 

Grun Von Jolk Rebekka ni Mkurugenzi wa mradi huo na anasema “kuwezesha wanawake kufanya kazi, tena kwa ufanisi ni jambo la msingi katika kupunguza umaskini. Na ni muhimu katika kuendeleza nguvu kazi kwa kuwa tunafahamu fedha anayopokea mama kwa kawaida inakwenda kwa watoto na hivyo ni sawa na kuwekeza kwenye nguvu kazi.” 

Hadi mwisho wa mwaka 2019 vituo 20 vya malezi ya watotovyenye uwezo wa kuhudumia watoto 24 kila kimoja, vilikuwa vimeanzishwa na sasa wanawake wanaweza kutunza akiba ya fedha wanazopata na kuwekeza kwenye miradi midogo midogo. 

Audio Credit
UN News/Jason Nyakundi -Ripota Kenya
Audio Duration
2'54"
Photo Credit
UNICEF/Agron Dragaj