Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tahadhari kabla ya hatari kunusuru mali na uhai Bangladesh 

Tahadhari kabla ya hatari kunusuru mali na uhai Bangladesh 

Pakua

Nchini Bangladesh, shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo, FAO limechukua hatua kusaidia wakulima na wafugaji kuepuka madhara makubwa ya majanga ya kiasili kama vile mafuriko ambayo yamekuwa yanakumba mara kwa mara taifa hilo na kusababisha wakulima na wafugaji kupoteza siyo tu mifugo yao bali pia chakula cha mifugo, mazao na makazi yao na hivyo kuwaacha katika lindi la umaskini. Jason Nyakundi na maelezo zaidi.

Eneo la Kurigram nchini Bangladesh, nyumbani kwa Morjina Begum, ambapo analisha mifugo yake katika zizi lao.

Morgina ni miongoni mwa maelfu ya wakulima nchini Bangladesh ambao mara kwa mara huathiriwa na majanga ya asili. Kama wanawake wengine nchini humo jukumu lao ni kutunza mifugo huku waume zao wakihudumia mashamba. 

Hata hivyo mwaka 2020, kijiji chao kilichoko ndani zaidi kaskazini-magharibi mwa Bangladesh kilikumbwa na mafuriko mabaya zaidi kuwahi kukumba eneo hilo katika kipindi cha miaka 35. 

Ingawa aliweza kuokoa karibu mifugo yake yote, nyumba na mashamba yao vilisombwa. 

FAO kwa kutambua umuhimu wa mifugo kwa lishe na kipato cha familia kama ya Morjina, mwezi Julai mwaka jana iliingilia kati mapema kabla ya mafuriko kupitia mradi wa hatua kabla ya Janga, AA ili wakulima waweze kujiandaa. 

Takwimu za awali zilipoonesha kuwa mito itajaa, FAO iligawa vyakula vya mifugo kwa kaya 19,000 zilizopo karibu na bonde la mto. 

“Chakula cha mifugo kilisaidia sana. Bila hiki chakula mifugo ingalikufa. Tunapata maziwa, mifugo ina afya, Kabla ya msaada huu, thamani ya ng’ombe kama huyu ilikuwa dola 235 lakini sasa imepanda hadi dola 471. Watoto wangu nao wananufaika wanakunywa maziwa na wanakuwa na afya.” 

Kwa upande wa wakulima nao wanapatiwa mbinu za kuhifadhi mazao yao na mbegu pindi maji ya mto yakionesha dalili za kujaa. 

Kupitia mfuko wa Umoja wa Matafa wa msaada wa dharura, CERF,  wakulima kama Munni Akhter wanapatiwa mapipa yasiyoingiza hewa ili kuhifadhi vitu muhimu zaidi kama vile mbegu, chakula na maji. 

Mapipa hayo yana uwezo wa kuelea kwa hiyo wakulima wanaweza kuondoka nayo pindi wanapolazimika kuhamia. Hii ina maana wakulima wanaweza kupanda mazao yao pindi hali itakapokuwa shwari na hivyo kuokoa mali na uhai. 

“Nilihifadhi maji kwenye pipa, kwa ajili ya kunywa na kupikia. Kwa kuwa nilikunywa maji safi, nimekuwa salama wakati wa ujauzito wangu.” 

Audio Credit
Grace Kaneiya/Jason Nyakundi
Audio Duration
2'41"
Photo Credit
NOOR for FAO/Sebastian Liste