Skip to main content

Jumuiya ya kimataifa na viongonzi mbalimbali wamuenzi Rais Magufuli

Jumuiya ya kimataifa na viongonzi mbalimbali wamuenzi Rais Magufuli

Pakua

Kifo cha Rais wa Tanzania John Magufuli kimegusa viongozi mbalimbali ukiwemo Umoja wa Mataifa, mashirika yake na marais na hata viongozi wastaafu kama anavyosimulia Flora Nducha katika taarifa hii baada ya kurambaza kwenye mitandao ya kijamii. 

(Taarifa ya Flora Nducha) 

Salamu za hivi karibuni zaidi za rambirambi zinatoka Umoja wa Mataifa ambako Tanzania ni mmoja wa wanachama. 

Katibu Mkuu wa Umoja huo, Antonio Guterres kupitia taarifa iliyotolewa leo jijini New York, Marekani, ameeleza kushtushwa na taarifa za kifo cha Rais John Magufuli na ametuma salamu za rambirambi kwa familia yake, seriali na wananchi wa Tanzania. 

Kupitia mtandao wa Twitter Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO,  Dkt. Tedros Ghebreyesu amesema, “salamu zangu za dhati za rambirambi kwa wananchi na serikali ya Tanzania kufuatia kifo cha Rais John Magufuli. Fikra zangu ziko na familia na taifa wakati huu wa kipindi kigumu.” 

Kutoka Somalia, akiandika kwa lugha ya Kiswahili,  Rais Mohammed Farmaajo amesema kwa niaba yake na kwa niaba ya serikali na taifa la Somalia, “ningependa kuwasilisha rambirambi zetu kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumpoteza kiongozi Rais John Magufuli. Tunalitakia Taifa zima na seriklai Subra na utulivu katika kipindi hiki cha maombi na maombolezo.” 

Nchini Kenya Rais mstaafu Mwai Kibaki kupitia ujumbe wake amesema, “ni  kwa machungu makubwa nimepokea taarifa za kifo cha Rais wa Tanzania John Magufuli. Natuma salamu za rambirambi kwa familia, marafiki, Tanzania na Afrika Mashariki nzima, naoamba Mungu awapatie faraja katika kipindi hiki.” 

Tukisalia Kenya, Waziri Mkuu mstaafu wa nchi hiyo, Raila Odinga ambaye alikuwa swahiba wa mwendazake Magufuli, ameelezea kupokea taarifa za kifo kwa huzuni kubwa. “Rais Magufuli na familia yake wamekuwa marafiki wetu wa karibu kwa muda mrefu. Makiwa kwa familia ya hayati na watu wa Tanzania. Mungu ailaze roho yake mahali pema penye wema.” 

Na kutoka Uganda, Rais Yoweri Museveni ametuma salamu za rambirambi na kusema, “alikuwa kiongozi wa vitendo aliyeamini na kutekeleza uwezeshaji wa kiuchumi kwa nchi za Afrika MAshariki. Tunaungana na watanzania katika kuomboleza kifo cha mwana huyu wa Afrika aliyetukuka,” 

 

Audio Credit
UN news/Grace Kaneiya
Audio Duration
4'22"
Photo Credit
Muhiddin Michuzi