Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chondechonde tuendelee kutunisha mfuko wa mshikamano wa kimataifa:WHO

Chondechonde tuendelee kutunisha mfuko wa mshikamano wa kimataifa:WHO

Pakua

Mfuko wa kimataifa wa mshikamano wa kukabiliana na janga la corona au COVID-19 leo umeadhimisha mwaka mmoja tangu kuzinduliwa na kutoa ombi la kuendelea kutunishwa ili kuwasaidia wahitaji wengingi zaidi wakati huu janga likiendelea kuitikisa dunia. Flora Nducha na taarifa zaidi

(TAARIFA YA FLORA NDUCHA)

Kwa mujibu wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO tangu kuanzishwa kwake mfuko huo wa mshikamano umechangisha karibu dola milioni 250 kutoka kwa watu binafsi 661,000, makampuni na mashirika, fedha ambazo zimeisaidia WHO na washirika wake kukabilina na janga la COVID-19 kote duniani. 

Miongoni mwa msaada uliotolewa kupitia fedha hizo ni kwa WHO kupeleka vifaa vya kuokoa maisha, kufikisha taarifa na kuwezesha utafiti katika nchi mbalimbali kote ulimwenguni. 

Mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt. Adhanom Ghebreyesus amewashukuru wote waliosaidia kutunisha mfuko huo akisema “ Ninamshukuru kila mmoja, makampuni na mashirika kwa kuchangia mfuko huu wa mshikamano. Ukarimu wenu umeleta mabadiliko makubwa. Mfuko huo ukifikisha mwaka mmoja tumeshuhudia kile tunachoweza kutimiza wakati wa matatizo makubwa na uhitaji.” 

Pamoja na kuwashukuru wote waliochangia kutunisha mfuko huo, WHO imesema mwaka huu wa 2021 utahitaji dola zingine bilioni 1.96 ili shirika hilo liendelee kuratyibu hatua za kukabiliana na janga hilo kimataifa na zaidi ya asilimia 60 zitaelekezwa kwenye mahitaji ya fursa za upatikanaji wa nyenzo kwa ajili ya COVID-19 ikiwemo vipimo, matitabu na chanjo. 

"Tumefanikiwa mengi zaidi  kwa mwaka mmoja uliopita. Lakini kwa bahati mbaya, janga hilo bado liko mbali kumalizika na hatuwezi kuacha kukabiliana nalo. Tunakushukuru kwa michango yako na tunaomba msaada wako kuendelea ili tuweze kuishinda COVID-19. ” Ameongeza Dkt. Tedros. 

Mfuko huo unaowezeshwa na wakfu wa Umoja wa Mataifa na na Shirika la Umoja wa Mataifa na wakfu wa msaada wa Uswis uliundwa kama jukwaa la ubunifu ili kuwezesha kampuni binafsi, watu binafsi na mashirika mengine kuchangia moja kwa moja kwenye juhudi za WHO za kuzuia, kugundua, na kupambana na COVID-19 ulimwenguni kote. 

Tangu kuzuka kwa janga la COVID-19 WHO imesafirisha karibu vifaa milioni 250 ikiwemo vifaa vya kujikinga kama glavu , magauani, barakoa na vifaa tiba zikiwemo machine za oksijeni kwa nchi zaidi ya 150, kuimarisha maabara za kitaifa kwa msaada wa kiufunzi, kusambaza vipimo vya COVID-19 zaidi ya milioni 250, kuratibu upelekaji wa timu za wataalamu zaidi ya 180 na kuchangia msaada wa vitanda 12,000 kwenye wodi za wagonjwa mahututi kwenye nchi ambazo mifumo yake ya afya imezidiwa uwezo. 

Audio Credit
UN News/Flora Nducha
Audio Duration
2'53"
Photo Credit
WHO/P. Virot