Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sasa hakuna tena kubebeshana na mizigo kutwa nzima- Wanufaika wa mashine ya kisasa ya kukamua chikichi

Sasa hakuna tena kubebeshana na mizigo kutwa nzima- Wanufaika wa mashine ya kisasa ya kukamua chikichi

Pakua

Umoja wa Mataifa kupitia kituo chake cha biashara, ITC imejibu ombi la wanawake wajasiriamali mkoani Kigoma nchini Tanzania kwa kuwapatia mashine ya kisasa ya kukamua mawese na hivyo kupunguza siyo tu muda wa kukamua mafuta hayo kutoka saa 8 hadi mbili bali pia kupata mafuta yenye ubora zaidi. Assumpta Massoi na maelezo zaidi.

Vifijo na nderemo katika wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma, magharibi mwa Tanzania baada ya kikundi cha wanawake wajasiriamali cha kati ya Kinazi kukabidhiwa mashine ya kisasa ya kukamua mawese.

Shuhuda ni Mwamvua Mrindoko Kaimu Mkuu wa mkoa wa Kigoma ambaye amesema, “nichukue fursa hii kuwashukuru wafadhili ambao ni ITC kupitia Kigoma Joint Programme, na SIDO pia niwapongeze sana kwa kuwa nimeona mashine hizi zimeandikwa SIDO Kigoma, kwa hiyo niwapongeze kwa hilo. Lakini lingine ni utunzaji kwa kuwa mashine hizi ni nzuri na ni mpya na zinafanya kazi vizuri na zote mmeziwasha hapa tumeshuhudia.”

Benta Sauja ni mwenyekiti wa kikundi hicho chenye wanachama 28 kilichoanzishwa mwezi Julai mwaka 2019 yeye anakumbuka hali ya zamani akisema, “miaka ya nyuma tumehangaika sana, unatembea na mizigo ya ngazi unaipeleka, unakamua unaanzia asubuhi  hadi jioni, unazunguka, ukikamua pipa moja unapata lita 25 tu za mafuta. Sasa hivi mashine hii inakamua vizuri tunapata mafuta ya kutosha, na bado hatuhangaiki unapeleka mzigo wako unatua na kazi ni kusimamia tu ni namna gani viende na  hakuna maumivu yoyote yale, hata mtoto hawezi kulia tena kuwa unamtuma nipelekee huu mzigo.” 

Katibu wa kikundi hicho Elisia Nzogela akamulika matarajio yao akisema wanategemea mafanikio kwa sababu walizoea mashine za kienyeji lakini walipojaribu mashine mpya waliona mafanikio ni mazuri. 

Kwa mhasibu wa kikundi Leokadia Raphael furaha yake ni ubora wa mafuta akisema kuna utofauti kabisa kwa kuwa mashine mpya inakamua vizuri na makapi yake yanakuwa meupe lakini yale ya mashine ya kienyeji mtu unazunguka hadi unachoka na unaamua kumwaga hata kabla chikichi hazijalainika vizuri. Halikadhalika amesema katika muda wa kati ya dakika 12 hadi 15 pipa moja linakuwa limeshakamuliwa na mchakato wa kuchemsha mafuta unaanza.



 

Audio Credit
Flora Nducha/Assumpta massoi
Audio Duration
2'33"
Photo Credit
ITC VIDEO