Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nuru ya elimu yaangazia watoto wakimbii wa ndani Niger

Nuru ya elimu yaangazia watoto wakimbii wa ndani Niger

Pakua

Mkakati wa kimataifa wa 'elimu haiwezi kusibiri' ECW,  leo umetangaza msaada wa dola milioni 1 kwa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR ili iwasaidie Watoto waliotawanywa na jamii zinazowahifadhi nchini Niger. Anold Kayanda na maelezo zaidi.

Kwa mujibu wa UNHCR mfumo wa elimu nchini Niger unakabiliwa na changamoto kubwa ikiwemo janga la corona au COVID-19, mabadiliko ya tabianchi, usalama mdogo, mashambulizi ya watu wenye silaha dhidi ya shule na sababu zingine na vinawasukuma maelfu ya wavulana na wasichana ambao ni wakimbizi na wakimbizi wa ndani kuacha shule. 

 

Na ili kushughulikia mara moja changamoto hizo na kuisaidia Niger kutimiza malengo yake ya elimu jumjuishi na kwa wote kama ilivyoainishwa kwenye malengo ya maendeleo endelevu, ndio maana leo mkakati wa elimu haiwezi kusubiri (ECW) umetangaza kutoa msaada wad ola milioni 1 kwa UNHCR nchini Niger. 

 

Akitangaza msaada huo mkurugenzi wa elimu haiwezi kusubiri Yasmine Sherif amesema “Watoto na vijana barubaru  na jamii zinazowahifadhi katika maeneo ya Tillabéri na Tahoua wanakabiliwa na madhila makubwa. Sote tunaweza kuchukua hatua kusaidia  na mkakati wa elimu haiwezi kusubiri  unashirikiana na UNHCR Niger ili kuunga mkono juhudi zake za kufikisha elimu na ulinzi.” 

 

Naye mwakilishi wa UNHCR Niger Alessandra Mprelli kwa upande wake amesema “Mwanzo wa mwaka huu 2021 umekuwa mgumu sana kukiripotiwa mashambulizi kadhaa ambayo yamewalazimisha maelfu ya watu kufungasha virano na hivyo kuwanyima elimu maelfu ya Watoto. Elimu bila shaka ni nyenzo muhimu ya kuwalinda Watoto na vijana walioathirika na vita , dhidi ya vifo, kujeruhiwa na kunyanyaswa. Pia elimu inawaondolea athari za kisaikolojia kwa kuwapa njia ya msaada, utulivu na mustakbali bora. Tunashukuru sana kwa msaada wa ECW.” 

 

Fedha hizo zitawafikia kwa msaada watoto 6,000 wasichana kwa wavula walioathirika na machafuko katika majimbo ya Tillabéri na Tahoua Niger na zitatumia kuweka miundombinu ya maji na usafi kwa ajili ya kujilinda na COVID-19, ujenzi wa madarasa, kuajiri waalimu, kutoa mafunzo kwa waalimu na wanafunzi na kununua vifaa vinavyohitajika. 

 

Niger inahifadhi jumla ya wakimbizi na wakimbizi wa ndani 573,059 kwa mujibu wa takwimu za UNHCR.

 

Audio Credit
Flora Nducha/Anold Kayanda
Audio Duration
1'44"
Photo Credit
© UNICEF/Juan Haro