Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanawake masikini wapatiwe ujira wakati huu wa COVID-19- UN

Wanawake masikini wapatiwe ujira wakati huu wa COVID-19- UN

Pakua

Pato la msingi la muda mfupi (TBI) likitolewa kwa mamilioni ya wanawake katika nchi zinazoendelea duniani linaweza kuzuia kuongezeka kwa umasikini na kupanuka kwa pengo la usawa wa kijinsia wakati huu wa janga la corona au COVID-19, imesema ripoti mpya iliyotolewa leo na shirika la mpango wa maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP). Jason Nyakundi na maelezo zaidi.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo wanawake wameathirika zaidi na janga la COVID-19  kuliko wanaume, kwa kupoteza mapato na kuondoka kwenye soko la ajira kwa kiwango kikubwa na kisha kugeukia sehemu kubwa ya kazi za malezi au kutoa huduma.  

Kwa mantiki hiyo ripoti imetoa wito kwa nchi wa kuanzishwa mara moja kwa pato la msingi la muda kwa misingi ya kijinsia kwa ajili ya wanawake masikini na wasiojiweza katika nchi zinazoendelea , ikisisitiza kwamba hatua hiyo ya dharura ni muhimu ili kuhakikisha wanawake walioathirika kiuchumi na janga hilo wanaweza kumudu maisha wakati huu wa corona. 

Akisisitiza hilo Mtawala Mkuu wa UNDP Achim Steiner amesema “serikali zinaweza kuchukua hatua sasa hivi kuelekeza asilimia 0.7 ya pato lake la taifa ,GDP kila mwezi kwa wanawake wanaokabiliwa na changamoto kubwa za kiuchumi na kijamii, kwa sababu pato la msingi la kila mwezi litahakikisha wanaweza kuishi wakati huu mgumu. Na faida za uwekezaji huo hazitowasaidia wanawake tu na familia zao, kumudu janga hili bali pia zitawawezesha wanawake hao kufanya maamuzi huru kuhusu fedha na chaguo la maisha yao.” 

Ripoti hiyo iliyotolewa kuelekea siku ya wanawake duniani itakayoadhimishwa Machi 8, imependekeza mkakati huo kwa wanawake wenye umri wa kufanyakazi kuanzia miaka 15 hadi 64 katika nchi zinazoendelea. 

Imeongeza kuwa kwanza unaweza kutoa usalama na uhakika wa kipato kwa muda mfupi kwa  wanawake milioni 613 wenye umri wa kufanyakazi ambao sasa wanaishi katika umasikini huku wakitengeneza njia ya uwekezaji kwa siku zijazo, na pili utapunguza madhila kwa wanake hadi bilioni 2 katika nchi zinazoendelea

Kwa mujibu wa ripoti faida nyingine kubwa ya TBI ni kwamba itapunguza pengo baina ya wanawake na wanaume wanaoishi katika umasikini kwa kuwapa wanawake uhuru wa kiuchumi na kuleta uwiano katika kudhibiti rasilimali ndani ya familia. 

“Pengo la usawa wa kijinsia linaendelea kupitia kutokuwepo uwiano wa kipato na mgawanyo wa kazi, na ingawa TBI sio suluhu ya moja kwa moja, lakini itawasaidia wanawake kuongeza haki ya chaguo wakati huu wa COVID-19” amesema Raquel Lagunas mkurugenzi wa timu wa masuala ya jinsia kwenye shirika la UNDP. 

Ameongeza kuwa TBI inatoa fursa ya utulivu wa kiuchumi kwa wanawake ili waweze kupanga maisha yao kwa ajili ya matakwa yao, mahitaji yao na kushiriki kikamilifu katika jamii zao.

Audio Credit
Flora Nducha/ Jason Nyakundi
Audio Duration
2'42"
Photo Credit
WFP/Rein Skullerud