Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kilimo hifadhi ndio mkombozi wetu- Wakulima Kigoma Tanzania

Kilimo hifadhi ndio mkombozi wetu- Wakulima Kigoma Tanzania

Pakua

Kilimo hifadhi kinaturejesha ujana – Wanufaika Kigoma- TV

Nchini Tanzania mafunzo ya kilimo hifadhi yaliyotolewa mwaka jana na shirika la chakula na kilimo la Umoja wa MAtaifa, FAO kwa wakulima mkoani Kigoma yameanza kuzaa  matunda na wakulima ndio mashahidi. Assumpta Massoi na maelezo zaidi. 

Mkulima Merina Siganigwa mnufaika wa mafunzo ya kilimo hifadhi yaliyotolewa na FAO kwa wakulima wa kata ya Muzye wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma akitoa ushauri kwa mkulima jirani yake.

Yeye na wenzake kupitia mashamba darasa walijifunza kilimo hifadhi kisichosumbua udongo, kuandaa mashimo kwa kufuata vipimo sahihi, kuweka samadi au mbolea za viwandani , na kuotesha mbegu tatu katika shimo moja badala ya mbili au moja. 

Boniface Yareheze ni mnufaika mwingine. “Mashimo ya kilimo hifadhi huwa na uwezo wa kuhifadhi unyevu hivyo kutoa fursa kwa mmea kukua haraka na kwamba, palizi ya kilimo hifadhi ni rahisi na haisumbui mizizi ya mmea.  Kilimo  hifadhi hukupatia mavuno mengi katika eneo dogo kulinganisha na kilimo cha kawaida. Kilimo hiki hakichoshi na  kinaturejeshea ujana kwa kuwa badala ya kutumia jembe la mkono kupalilia kwa mkono, unachukua kinyunyizi na kumwaga sumu ya kuua magugu.”

Boniface akatofautisha, “Pamoja na kutumia mbolea ya samadi na mbegu zinazofanana katika maeneo yanayofanana, kilimo hifadhi kimeonesha kuwa na mimea yenye afya na matumaini ya mavuno Bora huku kule ambako tumetumia kilimo cha kawaida mavuno ni hafifu.”

Mamiro Kitumbo afisa ugani kata ya Muzye na ana ushauri kwa wakulima. Anasema mkulima, “anaandaa kilimo wakati wa kiangazi ambapo kazi zinakuwa zimepungua. Akishaandaa kila kitu inaponyesha mvua, anapanda anakuwa na muda mrefu wa kupumzika. Sana sana kazi aliyobaki nayo ni kwenda kukagua kama kuna wadudu au madhara yoyote yaliyojitokeza shambani.”

Mafunzo hayo ya kilimo hifadhi ni sehemu ya Programu ya pamoja ya Kigoma, KJP inayotekelezwa na Umoja wa Mataifa kupitia mashirika yake kama FAO kwa ushirikiano na serikali ya Tanzania.
 

Audio Credit
Flora Nducha/Assumpta massoi
Audio Duration
2'16"
Photo Credit
UN News/Assumpta Massoi