Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wahamiaji Amerika ya Kati waathirika zaidi na njaa - WFP

Wahamiaji Amerika ya Kati waathirika zaidi na njaa - WFP

Pakua

Janga la njaa limeongezeka karibu mara nne katika miaka miwli iliyopita nchini El Salvador, Guatemala, Honduras na Nicaragua na kuwaacha takriban watu milioni 8 katika eneo hilo la Amerika ya Kati wakihitaji msaada mwaka huu wa 2021, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula WFP.  Jason Nyakundi na maelezo zaidi.

Kwa mujibu wa WFP njaa imetokana na mgogoro wa kiuchumi uliochangiwa na janga la corona au COVID-19 na miaka ya majanga mengine ya mabadiliko ya tabianchi yakiwemo mafuriko na vimbunga. 

Hali ni mbaya zaidi nchini Honduras ambako kuna idadi kubwa ya watu wanaohitaji msaada wa dharura wa chakula.  

Wahamiaji waathirika zaidi

Miongoni mwao ni mhamiaji Marlene na mumewe ambao walipoteza kazi zao sababu ya COVID-19 na kulazimika kuwa vibarua wa siku mjini Saint Barbara, lakini kimbunga Iota  kilipopiga Amerika ya Kati Novemba mwaka jana hata hivyo vibarua vya siku vikaota nyasi. 

Sasa wanalazimika kukusanya vipande vya mabati kuukuu na kuuza wakipata senti 8 za Kimarekani kwa siku ili wanunue chakula cha watoto wao wanne na ikishindikana wanageukia kuchuma mimea ya porini kama Yerba Mora kuwa mbadala wa mlo. Kwa uchungu mkubwa anasema,“Kukipatikana hata chakula kidogo tu cha kuwatosheleza watoto, basi inakuwa ni kwa ajili yao hata kama sisi tutalala njaa, unajua kwamba kama mzazi cha msingi ni watoto kula kuliko sisi.” 

Marlene na mumewe walijaribu kukimbia na watoto wao kama maelfu ya watu wengine ili kwenda kusaka mustakbali bora nchi jirani, lakini ndoto zao zilizizima pale waliporejeshewa mpakani. 

Watu milioni 6.8 wamepoteza kila kitu kutokana na vimbunga na ajira zimetoweka sababu ya COVID-19, mkombozi wao pekee aliyesalia ni WFP. Miguel Barreto ni mkurugenzi wa kanda hiyo wa WFP “Kwa mujibu wa utafiti wetu sasa asilimia 15 ya watu wanafikiria kuhama na tukilinganisha na idadi ya mwaka 2018 ilikuwa asilimia 8 tu na tukilinganisha katika nchi moja kama Honduras ,nchini humo asilimia 17 ya watu wanafikiria kuhama sababu ya mgogoro huu. Hivyo WFP iko tayari kuendelea kuzisaidia nchi hizi. Tunapanga kuwafikia watu milioni 2.6 mwaka huu 2021 na tunahitaji dola milioni 46 kuziba pengo hilo.” 

WFP imetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kusaidia juhudi za shirika hilo Amerika ya Kati ili liweze kufikisha msaada wa dharura wa chakula cha kuokoa maisha. 

 

Audio Credit
Flora Nducha/ Jason Nyakundi
Audio Duration
2'37"
Photo Credit
WFP/Carlos Alonzo