Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola 1 iwekwezayo katika mlo shuleni huzalisha dola 9 - WFP

Dola 1 iwekwezayo katika mlo shuleni huzalisha dola 9 - WFP

Pakua

Mafanikio ya miongo kadha ya mgao wa chakula shuleni yaliyolenga watoto walio hatarini na wasio na uwezo wa kupata mlo bora, yako hatarini kutumbukia nyongo kutokana na janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19, imesema ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa hii leo huko Roma Italia ikimulika hali ya mpango wa mlo shuleni duniai, SOSFW. Assumpta Massoi.

Nchini Madagascar, wafanyakazi wakiwa katika shamba la mazao yanayotumiwa shuleni huku wengine wakisagisha mihogo hiyo ambayo hupikwa na kupatiwa watoto shuleni.
WFP katika ripoti yake ya leo inasema duniani kote COVID-19 ilipora watoto milioni 370 haki ya kupata mlo shuleni kwa kuwa shule zilifungwa.

Na sasa WFP inataka hatua za dharura kurejesha huduma hiyo kama ilivyokuwa inatolewa kabla ya COVID-19 na kupanua zaidi ili kufikia watoto wengine milioni 73 ambao walikuwa hawafikiwi na mpango wa mlo shuleni kabla janga la Corona kuibuka.

Akizungumzia ripoti hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa WFP, David Beasley amesema “mpango wa mgao wa mlo shuleni umeleta mabadiliko makubwa . Huo mlo mmoja kwa siku ni sababu kwa watoto wenye njaa kutaka kwenda shuleni. Halikadhalika ni kichocheo kizuri cha kuhakikisha watarejea shuleni hata vizuizi vya kufungwa shule vitakapoondolewa. Tunahitaji programu kama hizi zianze tena na ziwe bora zaidi kuliwa awali na hatimaye tuondokane na COVID-19 kuvuruga mustakabali wa mamilioni ya watoto walio hatarini sehemu mbalimbali duniani.

Mwaka 2021, WFP imesema itajenga ubia kusaidia serikali kuimarisha mipango ya mgao wa mlo shuleni.
Kati ya mwaka 2013 na 2020, idadi ya watoto waliopata mlo shuleni iliongezeka duniani kote kwa asilimia 9 na katika nchi nchi za kipato cha chini ongezeko lilikuwa asilimia 36, kwa kuwa serikali zilipanua wigo wa miradi hiyo na kufanya mgao wa chakula shuleni kuwa mradi wa wa kina zaidi wa hifadhi ya kijamii duniani.

Tafiti zimeonesha kuwa kwa maisha ya mtoto kutoka familia maskini, mlo shuleni unaweza kuwa na mchango mkubwa na kwa watoto wa kike manufaa hayo ni dhahiri zaidi kwa kuwa wanabakia shuleni muda mrefu, viwango vya ndoa katika umri mdogo vinapungua halikadhalika ujauzito katika umri mdogo.
Ripoti ya WFP inasema kuwa mpango wa mlo shuleni unapotumia mazao yaliyolimwa kwenye jamii husika huchochea uchumi wa jamii. 
“Huongeza mahitaji ya milo tofauti, mlo wenye lishe na kuweka hakikisho la soko na kusaidia kilimo cha eneo husika na kuimarisha mifumo ya chakula ya jamii.”
Kwa mujibu wa ripoti hiyo mipango ya mlo shuleni inaleta faida kubwa ya hadi dola 9 kwa kila dola 1 inayowekezwa kwenye mradi huo. 

Halikadhalika huotoa fursa ya ajira ambapo kwa mujibu wa WFP ajira mpya 1,668 huanzishwa kwa kila watoto 100,000 wanaolishwa chakula shuleni.
 

Audio Credit
Flora Nducha/Assumpta massoi
Audio Duration
2'46"
Photo Credit
UNICEF/Francis Emorut