Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Theluji pasi kifani yatishia maisha ya wakimbizi Lebanon

Theluji pasi kifani yatishia maisha ya wakimbizi Lebanon

Pakua

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limesema hali mbaya ya hewa inayoambatana na majira ya baridi kali  yaliyoghubikwa na kumwagika kwa theluji nyingi Mashariki ya Kati, imeongeza zahma kwa mamilioni ya wakimbizi na wakimbizi wa ndani kama inavyofafanua taarifa ya Jason Nyakundi 

Nchini Lebanon katika makazi yasiyo rasmi ya wakimbizi kwenye bonde la Beka theluji inamiminina pasi kifani, na kusababisha athari kwenye zaidi ya  asilimia 70 ya makazi haya kutokana na theluji kulundikana au mahema kuvuja. 

UNHCR inasema maelfu ya wakimbizi wameathirika na kiasi kikubwa cha theluji iliyoanza kumwagika tangu Februari 12 nchini Lebanon na kusababisha baridi kali, mvua kubwa, barafu na upepo mkali. 

Mahema mengi katika makazi ya bonde la Bekaa yamejengwa kwa maturubahi na hivyo mengi yanavuja na mengine kuzidiwa uzito na  theluji na kuporomoka. Mafuriko nayo yanayoambatana na theluji hiyo yaningia mpaka ndani ya mahema . 

Shirika hilo la wakimbizi linasema hofu yake kubwa ni kwa wale ambao hawana huduma muhimu kama majiko ya kupasha joto mhema yao, lakini pia kwa waliopoteza mahema yao baada ya kuporomoka kwani wamesalia bila makazi na inabidi kujibanza kwa  wakimbizi wengine ili kunusuru maisha yao kutokana na baridi kali nje.

Hali hiyo UNHCR inasema inaweka afya wakimbizi hao katika hatari kubwa  na hivyo hatua za haraka zinahitajika kuwanusuru na janga juu ya janga. 

Kwa kushirikiana na mamlaka ya Lebanon na wadau wengine wa misaada UNHCR imeanza kupeleka msaada wa dharura ikiwemo mavazi ya baridi, vifaa vya kupasha moto mahema, ukarabati wa mahema hayo na misaada mingine ya lazima kuweza kuwavusha wakimbizi hao kwa wakati huu wa baridi kali. 

Audio Credit
Flora Nducha/JAson Nyakundi
Photo Credit
UNICEF/Alessio Romenzi