Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Athari za mabadiliko ya tabianchi ni 'mwiba' kwa watoto- UNICEF

Athari za mabadiliko ya tabianchi ni 'mwiba' kwa watoto- UNICEF

Pakua

Mwakilishi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, nchini Msumbiji Maria Luisa Fornara akitembelea eneo la Guara Guara ambayo sasa ni makazi ya walioathiriwa na kimbunga Eloise, amesema inasikitisha kuona watoto wakiteseka kwa mara nyingine kutokana na matokeo mabaya ya mabadiliko ya tabianchi.  Grace Kaneiya na maelezo zaidi.

Kwa sababu ya mafuriko, familia zililazimika kukimbia Buzi, moja ya maeneo yaliyoathiriwa zaidi na kimbunga Eloise kilichoipiga Msumbuji mwezi uliopita kwenda mbali na nyumba zao hadi katika eneo la Guara Guara ambapo watoto takribani 8000 na familia zaoa, hapa, pamoja na malazi, wanapata pia maji salama, chakula, huduma za afya na vifaa vya shule ili waweze kuendelea na masomo yao kwani walivyokuwa navyo awali vilisombwa na maji.  

Mwakilishi UNICEF nchini Msumbiji, Maria Luisa Fornara amelitembelea eneo hili akiwa wadau wengine wanaojihusisha na masuala ya afya, usafi na kujisafi, pamoja na miundombinu. Bi Fornara anasema,  "Kama matokeo ya ongezeko la joto duniani, nchi kama Msumbiji zinaathiriwa zaidi na dhoruba na dhoruba hizi zinazidi kuimarika. Ni muhimu sana kuwekeza zaidi katika kupunguza hatari za majanga ili familia hizi ziweze kukabiliana na majanga haya.” 

Akielezea alichokishuhudia baada ya kuzunguka katika kambi zilizojengwa kwa mahema anasema, tuko hapa Guara Guara kwenye sehemu ya juu ambapo familia nyingi ambazo Kimbunga Eloise kiliwaathiri huko Buzi zimepata kimbilio. Kama unavyoona, familia hizi zinahitaji sana maji na usafi wa mazingira, ulinzi, lishe, huduma ya matibabu, na zinahitaji pia makazi. Mwakilishi huyo wa UNICEF anaongeza akisema,  "Inatia uchungu kuona kwamba watoto hawa wanateseka tena na janga kubwa baada ya miaka miwili tu baada ya Kimbunga Idai kuikumba nchi hii." 

Eloise ni kimbunga kilichoipiga Msumbiji mnamo tarehe 23 mwezi uliopita yaani Januari, kikiwa na upepo wenye kasi ya kufikia kilomita 160 kwa saa. 

Audio Credit
FLORA NDUCHA/ GRACE KANEIYA
Photo Credit
UNICEF Mozambique/Ricardo Franco