Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali tete wakimbizi wa ndani nchini Burkina Faso

Hali tete wakimbizi wa ndani nchini Burkina Faso

Pakua

Dharura kubwa ya kibinadamu inajitokeza nchini Burkina Faso ambapo kuongezeka kwa ukosefu wa usalama na mizozo katika kipindi cha miaka miwili iliyopita kumesababisha mzozo unaokua kwa kasi zaidi wa makazi, watu zaidi ya milioni wakifurushwa kutoka katika makazi yao. Taarifa ya Ahimidiwe Olotu, inaeleza zaidi. 

Naibu Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA, Ramesh Rajasingham katika ziara yake nchini Burkina Faso amekutana na jamii kadhaa zilizoathiriwa na vurugu na kulazimika kuyakimbia makazi yao. 

Katika mji wa tano kwa ukubwa Burkina Faso, Kaya, ulioko kaskazini mashariki mwa mji mkuu Ouagadougou, kuna kituo cha wakimbizi wa ndani ambao wamezikimbia ghasia katika maeneo yao nchini humo. 

 

Waliofanikiwa kukikimbia kifo wamekimbilia hapa na wanasaidiwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa. Mmoja wa wakimbizi hao wa ndani ni Mouniratou Maiga anaeleza kilichomkimbiza, 

(Sauti ya Mouniratou Maiga)-TABORA 

“Siku moja walikuja na bunduki, wakaua wanaume wanne na kisha wakarejea tena hawakuwakuta wanaume kwa hivyo wakawapiga wanawake, hicho ndicho nilichokiona. Ndio maana tukaja hapa.” 

Sayouba Sawadogo, mwanaume mkimbizi naye anasema, “nilikuja hapa Kaya kwa miguu. Nilikaa kichakani kwa siku tatu kisha nikaja hapa kwa miguu. Nilipofika nililala nje kwa kuwa sikuwa na chochote, sikuwa na pesa ya kukodi nyumba, hakuna wa kunisaidia. Niko hapa na mke wangu, tulikaa chini ya mti.” 

Mahitaji ya kibinadamu yameongezeka sana Burkina Faso, na takwimu zinaonesha watu milioni 3.5 watahitaji msaada wa kibinadamu katika mwaka huu 2021. Matatizo ya kibinadamu nchini Burkina Faso yamezidishwa zaidi na janga la COVID-19. Naibu Mkuu wa OCHA, Ramesh Rajasingham,  akiwa ziarani kwenye kambi hii anasema, "tumekuwa na zaidi ya watu milioni moja waliokimbia makazi yao kwa miezi kama kumi na mbili hivi karibuni, kwa hivyo Burkina Faso ni janga jipya ikiwa imetembelewa na matatizo mengine kama hayo, wasiwasi na vurugu na msimamo mkali ambao tumeona tayari katika sehemu nyingine ya Sahel kama vile Mali na Niger. Matokeo yake, watu nahofia maisha yao, wanaacha nyumba zao na mifugo, wanakimbia na chochote walichonacho kuja katika maeneo yenye msongamano za Burkina Faso kama hapa Kaya, mji ambao umewapokea maelfu ya wakimbizi wa ndani.”  

Audio Credit
Flora Nducha/Ahimidiwe Olotu
Audio Duration
3'19"
Photo Credit
UNOCHA/Otto Bakano