Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Programu ya UNICEF ya elimu kwa njia ya redio yaokoa watoto wakimbizi Cameroon

Programu ya UNICEF ya elimu kwa njia ya redio yaokoa watoto wakimbizi Cameroon

Pakua

Kuelekea siku ya radio duniani tarehe 13 mwezi huu wa Februari, tunakwenda nchini Cameroon ambako mradi wa mafunzo ya elimu kwa njia ya redio yamekuwa jawabu kwa maelfu ya watoto waliofurushwa makwao kutokana na ghasia kwenye maeneo ya kusini-magharibi na kaskazini-magharibi mwa nchi hiyo.. Assumpta Massoi na maelezo zaidi.

Mashambulizi katika maeneo ya kusini-magharibi na Kaskazini-magharibi mwa Cameroon yamesababisha maelfu ya watu kukimbia makwao na miongoni mwao ni watoto., hali inayofanya wakose haki yao ya msingi ya elimu.

Katika kuhakikisha kuwa wanapata huduma hiyo mfuko wa dharura wa Umoja wa Mataifa, CERF kupitia shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF umefanikisha mradi uliowezesha watoto 3,500 wakiwemo wakimbizi wa ndani kupata elimu.

Elimu ni kupitia matangazo ya redio katika wilaya za Fako na Meme kwenye mkoa wa Kusini-Magharibi kama anavyosema Njaku George mratibu wa mradi huo mkoani humo.

Bwana George anasema, “Idadi kubwa ya hawa watoto wanatoka porini na vijiji ambavyo vimetiwa moto na wako katika eneo hili. Watoto wamefurahi sana kuwepo katika maeneo haya salama tuliyoandaa ya kujifunza. Kama unavyoona hapa tuko Isokolo, moja ya maeneo na vituo ambako tunatekeleza mradi wa mafunzo kwa njia ya redio na watoto. Watoto wengi wamejifunza na wazazi wamekiri na kusema kuwa watoto  ambao hawakujua kusoma kwa miaka mitatu sasa wanaweza kusoma na hata kuzungumza kiingereza. Asante sana UNICEF.”

Miongoni mwa wanufaika ni Tanya mwenye umri wa miaka 11 ambaye alitenganishwa na wazazi wake kutokana na ghasia na hajahudhuria shule kwa miaka mitatu.

Mwingine ni Favour mwenye umri wa miaka 11 ambaye naye tangu shule yao iliposambaratishwa, yeye na familia yake walikimbia kijiji chao na hajakuwepo shuleni, lakini sasa mradi wa kujifunza kwa njia ya radio umekuwa mkombozi.

 

Audio Credit
Grace Kaneiya/Assumpta Massoi
Audio Duration
2'1"
Photo Credit
© UNICEF/Salomon Marie Joseph Beguel