Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Licha ya COVID-19 UNICEF yaendelea kusaidia mama na mtoto Uganda

Licha ya COVID-19 UNICEF yaendelea kusaidia mama na mtoto Uganda

Pakua

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, mapema mwezi huu limepokea shehena ya vifaa tiba mbalimbali vya kusaidia afya ya mama na mtoto nchini Uganda. Taarifa ya mwandishi wetu wa Uganda, John Kibego inaeleza zaidi. 

Ndege aina ya Airbus A330-800 ya shirika la ndege la Uganda inaonekana ikipokelewa kwa heshima ya kumwagiwa maji inapowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe. 

Ndege hiyo imebeba mzigo wa UNICEF ambao unaletwa Uganda kusaidia afya ya akina mama na watoto.  

Mzigo uliomo katika ndege hii ni pamoja na vifaa muhimu vya kufuatilia hali ya akina mama na watoto wachanga wakati wa ujauzito, wakati wa kujifungua na kipindi cha baada ya kujifungua. Pia kuna vifaa vya kusaidia watoto wachanga walio na ugumu wa kupumua wakati wa kuzaliwa na vifaa vya kusaidia kulisha watoto wachanga wadogo na wagonjwa katika Wilaya ya Isingiro, magharibi mwa Uganda.  

Wilaya ya Isingiro ni moja ya wilaya za Uganda zinazohifadhi wakimbizi. Vitu vilivyonunuliwa vilitegemea mahitaji kama yalivyooneshwa na kuombwa na mamlaka ya Wilaya ya Isingiro 

Pia katika vifaa tiba vilivyopokelewa ni pamoja na vipimo vya mzingo wa mkono kwa ajili ya mpango wa lishe na pia mavazi maalumu kwa ajili ya kujikinga na ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona, yaani Covid-19.  

Usafirishaji wa vifaa hvyo umeratibiwa na taasisi ya Global Logistics Cluster kwa kushirikiana na wakfu wa kampuni ya Airbus. 

 

Audio Credit
Flora Nducha/John Kibego
Audio Duration
1'20"
Photo Credit
UNICEF/Jimmy Adriko