Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkulima aibuka na mbinu za kuepusha wanyamapori kuvamia mashamba yao

Mkulima aibuka na mbinu za kuepusha wanyamapori kuvamia mashamba yao

Pakua

Kutana na mkulima kutoka Zimbabwe ambaye kupitia miradi ya shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo FAO anajaribu kwa kila njia kuhakikisha mfumo wa kilimo unaboreka lakini pia wakulima wa jamii yake  wanalinda mazingira na kuishi kwa amani na wanyamapori. Jason Nyakundi na maelezo zaidi.

Huyu ni mkulima mdogo Shupa Mushimba akiwa katika jimbo la Mucheni nchini Zimbabwe anasema maisha yake yanategemea sana kilimo na pia bustani lakini na mbali ya hapo anajihusisha na masuala ya maendeleo ya jamii, anawasaidia watu ili wasongembele pamoja. 

Katika jamii yake Shupa huwahamasisha wenzie kuboresha kilimo chao, kulinda mazingira na kuhifadhi wanyapori Kaskazini mwa Zimbabwe. 

Na kilimo ndio uti wao wa mgongo si kwa chakula tu bali kwa kipato pia, lakini si wakati wote wanaweza kukidhi mahitaji yao hata ya mlo wa siku kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo wadudu waharibifu wa mazao, migogoro kati ya wakulima na wanyamapori na ukame uliokithiri ambao huwaletea shida kubwa ya maji hasa kwa wakulima wa bustani kama Shupa,“Mara nyingi tunakwenda kuteka maji kwa kutumia makopo na ndoo kwa kawaida ni shughuli inayofanyika polepole na kwa sababu hiyo hatuwezi kulima bustani kwa kiwango kikubwa .” 

Na kwa mujibu wa Shupa hiyo sio changamoto peke yake, jirani zao wanyamapori ni mtihani mkubwa ,“Jamii yetu iko katikati ya mbuga mbili za taifa za wanyama, wakati mwingine wanyama hao wanakuja na hata kuharibu mazao yetu hususan tembo, na kwa mbuzi wetu adui mkubwa ni mamba, mwaka jana nilipoteza wawili, hivyo tunahakikisha mifugo yetu yote inafungiwa. Kisha wakati mwingine hata simba wanakuja” 

Kwa mujibu wa FAO, mipango bora ya matumizi ya ardhi, upatikanaji wa maji na ulinzi bora vinahitajika ili kulinda mifugo, mazao na kuhifadhi wanyamapori.  

Na kwa mantiki hiyo kupitia ufadhili wa Muungano wa Ulaya na kituo cha kimataifa cha mazingira cha Ufaransa FAO imeanzisha mradi wa udhibithi endelevu wa wanyamapori (SWM) ili kumsaidia Shupa na jamii yake kuimarisha kilimo, kupunguza mmomonyoko wa udongo, kuongeza mazao, kuboresha maisha na kuhakikisha wanaishi kwa amani na wanyamapori  ili hatimaye siku moja ndoto ya Shupa ya kuendesha kilimo kwa ajili ya biashara iweze kutimia.

Audio Credit
Flora Nducha/ Jason Nyakundi
Audio Duration
2'21"
Photo Credit
©FAO/Kenya Team